TIB yawaita wajasiriamali, wawekezaji kuchangamkia mikopo

NA MWANDISHI WETU, MWANZA       

BENKI ya Maendeleo Tanzania (TIB) imeitaka jamii kuchangamkia fursa za mikopo zinazotolewa na benki hiyo ili kuwekeza katika miradi ya maendeleo kwa ajili kuchagiza ukuaji wa uchumi nchini. 

Wito huo umetolewa na Afisa Uhusiano Mwandamizi wa Benki hiyo, Giusy Mbolile (pichani kushoto) kwenye maadhimisho ya 'Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa' yanayoendelea katika viwanja vya Rock City Mall jijini Mwanza. 

Mbolile alisema kuwa TIB ina wajibu wa kuwezesha upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu na wa kati kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi nchini, hivyo wawekezaji wenye miradi ya kimkakati wanapaswa kuitumia benki hiyo kufanikisha miradi yao. 

“Benki ya Maendeleo (TIB) ni taasisi ya serikali iliyoanzishwa kwa malengo ya kuwezesha upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu na wa kati kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi, hivyo nawasihi wawekezaji wenye miradi ya kimkakati kuitumia ili kufanikisha uwekezaji huo,” alisema Mbolile. 

Aliongeza kuwa benki hiyo inatoa mikopo kwenye sekta mbali mbali zikiwemo za viwanda, madini, huduma, miundombinu, nishati na maji pamoja na programu za mikopo ya wawekezaji wadogo na wa kati (SMEs).  

Aliongeza kuwa mikopo hiyo inatolewa ili kuchagiza ukuaji wa shughuli za kiuchumi ili kutekeleza mipango mbali mbali ya serikali inayolenga kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu nchini. 

Aliongeza kuwa benki inatumia maadhimisho hayo kusambaza taarifa na kujua mitazamo, kero na mahitaji ya taarifa za wadau wa benki hiyo ili kuiwezesha kuimarisha bidhaa na huduma zake.  

Maadhimisho hayo yaliyozinduliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk. Philip Mpango, yameanza Novemba 21 na kutarajiwa kukamilika Novemba 26, mwaka huu jijini Mwanza ikiwa ni utekelezaji wa mpango mkuu wa maendeleo ya sekta ya fedha wa mwaka 2020/2021 – 2029/2030 yakifanyika chini ya kauli mbiu ‘Elimu ya fedha kwa maendeleo ya watu’. 

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango