JUWAZA kuhamasisha upatikanaji haki za wazee

NA MWANDISHI WETU

JUMUIYA ya Wastasfu na Wazee Zanzibar (JUWAZA) imesema itaendelea kuhamasisha upatikanaji wa stahiki za wazee zikiwemo za kiafya  ili kupata haki zao na afya zao zinaimarika.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari ofisini kwake Migombani, Katibu wa jumuiya hiyo, Salama Kondo Ahmed, alisema jumuiya imekuwa ikitekeleza kazi zake kwa mashirikiano na serikali pamoja na taasisi binafsi katika kuhakikisha inafikia malengo yake.

Alisema kuwa idadi ya watu wenye umri wa miaka 80 na kuendela inakadiriwa kukua kwa mara tatu zaidi baina ya mwaka 2022 na 2050 na kufikia milioni 426 ulimwenguni hivyo nchi zinahitaji kujiandaa na kuandaa mazingira ya kukidhi mahitaji ya wazee.

Kondo alisema, JUWAZA ina mikakati mbali mbali ya kuimarisha ustawi wa wazee na wastaafu itakayotekelezwa kwa ushirikiano na serikali na taasisi binafsi

“Miongoni mwa mambo ambayo tumeweza kuyasimamia ni pamoja na kufanya utetezi na kupelekea kuuanzishwa kwa mpango wa pensheni jamii kwa wazee wote toka mwaka 2008 mpango ulioanza kutekelezwa 2016,” alisema Kondo.

 Alieleza kuwa na mpango huo ulioanza kutekelezwa mwezi Aprili, 2016 kwa wazee wenye umri wa kuanzia miaka 70 kupokea shilingi 20,000 kila mwenzi zoezi ambalo linaendelea hadi hivi sasa.

Alitaja mafanikio mengine ya jumuiya hiyo kuwa ni pamoja na kuundwa kwa mabaraza 342 ya wazee katika ngazi ya shehia Unguja na Pemba.

Hata hivyo, alisema kuwa wamefanya ushawishi kuhusu kuanzishwa kwa sheria ya wazee namba 2 ya mwaka 2020 kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ambayo iliwekwa saini mwezi Aprili 2020 na kuanza kutumika.

Kondo alisema kufuatia ongeeko kubwa la maradhi yasiyoambukiza miaka ya hivi karibuni kumekuwa na wadau hususani asasi za kiraia zimekuwa zikitoa huduma za maradhi hayo katika jamii.

“Pamoja na wingi wa wadau hawa lakini kumekosekana mashirikianao baina yao na hivyo mafanikio yanapatikana hayafikii kile kiwango kinachotakiwa,” alisema.

Pamoja na hayo, aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuendelea kushirikiana na jumuiya hiyo na kuwapa kipaumbele kila wanapohitaji kuonana na uongozi wa juu wa serikali pamoja na asasi za kiraia kwani imekuwa ikiwaunga mkono likiwemo shirika la Help Age Internation Tanzania (HAITAN).

Comments

Popular posts from this blog

ZAMECO yakerwa na video ya udhalilishaji mtandaoni

Airtel Foundation yazindua mpango wa udhamini wa masomo kwa vijana

SMZ yawaita vijana kushiriki kilimo