Utulivu watawala upigaji kura Amani

NA MWANDISHI WETU

MWENYEKITI wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Jacobs Mwambegele, amesema uchaguzi mdogo wa jimbo la Amani uliofanyika jana, umefanyika katika mazingira ya amani na kwamba tume yake imetimiza wajibu.

Akizungumza mara baada ya kukagua vituo mbali mbali kuangalia zoezi hilo linavyofanyika, Mwenyekiti huyo alisema vituo vyote vya kupiga kura vimefunguliwa kwa wakati na wapigara kura wamepata vifaa vyote.

Alisema vituo 23 vilivyotumika katika zoezi hilo kwa shehia nne vilifunguliwa saa 1:00 asubuhi na vilifungwa majira ya saa 10:00, ikiwa ni kuashiria kumalizika kwa zoezi la kumchagua mbunge mpya wa jimbo hilo.

Alisema katika vituo hivyo, mawakala wa vyama vya siasa, walipewa fursa kamili ya kutekeleza majukumu yao kwenye vyumba vya kupigia kura, huku wananchi nao wakijitokeza kwa wingi kushiriki kwenye zoezi hilo. 

Alisema hadi muda wa mchana wa jana, hakukua na malalamiko yaliyofikishwa katika tume hiyo na kwamba tume ilikuwa tayari muda wote kupokea changamoto.

Baadhi ya wagombea waliozungumza na gazeti hili walisema, uchaguzi huo umekwenda vizuri na kwamba ulikuwa uhuru na haki, licha ya kuwepo kwa changamoto ndogo ambazo walisema haziwezi kuathiri uchaguzi kwa ujumla wake.

Aliyekuwa mgombea kupitia CCM, Abdul Yussuf Maalim, aliyepiga kura katika kituo cha Kilimahewa Juu, alisema zoezi hilo linakwenda vizuri na wapiga kura wamejitokeza kwenda kupiga kura kwa wakati.

Alisema kwa upande wake zoezi aliliona kuwa linakwenda vizuri na kuwashauri wagombea wenzake endapo wanamalalamiko ya zoezi hilo kuripoti katika vyombo husika ili kuweza kupatia ufumbuzi kwa wakati.

Nae, mgombea kutoka ACT-Wazalendo, Mohamed Khamis Mohamed, alisema, zoezi hilo kwa upande wake halijaenda vizuri akidai kuwa wapiga kura walio wengi sio wakaazi wa jimbo hilo.

Aidha alisema kuwa kumekuwepo kwa madai ya wapiga kura wakishamaliza kupiga kura wanakwenda kufuta wino waliopakwa na tume hiyo na kuingia tena kwenda kupiga kura nyengine.

Kwa upande wake, msimamizi Msaidi wa Uchaguzi wa Jimbo la Amani, Ali Idarous Suleiman, alisema katika vituo vyao vyote vya kupigia kura zoezi limekwenda vizuri na wananchi wamejitokeza kwa wingi.

Akizungumzia suala la kuwepo kwa wapiga kura wanaodaiwa kuwa sio wakaazi wa jimbo hilo, alisema malalamiko hayo hayakuripotiwa kwani mawakala walipewa mafunzo endapo kutatokezea tatizo hilo kwenda kuliripoti wa wasimamizi wa uchaguzi. 

Jumla ya vyama vya siasa 14 vimesimamishwa wagombea katika uchaguzi huo ambapo kwa mujibu wa taarifa ya Mwenyekiti wa Tume hiyo, wakati akizungumzia na waandishi wa habari siku moja kabla ya kufanyika uchaguzi jumla ya wapiga kura 114,647 waliandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga.



Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango