Dk. Mwinyi ahimiza uzalishaji, ulaji mbogamboga, matunda
RAIS wa Zanzibar na Mweyekti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuna haja ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya mboga mboga na matunda ili kukidhi mahitaji ya soko la mazao hayo nchini.
Ameeleza hayo jana wakati akizindua kituo cha taarifa na maarifa ya kilimo cha mazao hayo (Horticulture) kilichopo Mpendae Kwa Binti Hamran, wilaya ya Mjini Unguja akisema Zanzibar inahitaji tani 276,000 kwa mwaka ili kukidhi mahitaji kwa wananchi wake.
Alisema takwimu zinaonesha kuwa kila mzanzibari anahitaji kilo 146 za mazao hayo kwa mwaka na kwamba uwepo wa hoteli za kitalii, inakadiriwa wastani wa tani 2,000 zinatumika kwa mwaka katika eneo hilo.
Aidha alisema Zanzibar ipo nyuma katika matumizi ya mboga na matunda hivyo anaamini wakulima wataongeza kasi ya uzalishaji wa kilimo cha mazao hayo kukidhi ukubwa wa mahitaji unaokua kila siku.
Dk. Mwinyi akipata maelezo kuhusu kilimo cha hortculture kutoka kwa mwanaharakati wa kilimo hai, Mwatima Abdallah Juma
Alifahamisha kuwa mwaka 2021/2022, uzalishaji wa mazao ya ‘horticulture’ Zanzibar ulifikia jumla ya tani 148,000 kiasi ambacho ni ongezeko la asilimia 68.2 katika kipindi cha mwaka 2012.
Alisema ongezeko la uzalishaji limepunguza utegemezi ambapo uagizaji wa matunda na mbogamboga kutoka nje ya nchi umepungua kutoka asilimia 80 mwaka 2014 hadi kufikia asilimia 26 mwaka 2021.
Alisema kilimo hicho pia ni muhimili wa lishe na afya bora kwa wananchi kwani utumiaji wa mazao ya mboga mboga, matunda na viungo huwapa virutubisho muhimu kwa ajili ya kujenga na kutunza miili na kutufanya wawe na afya njema.
Akizungumzia upatikanaji wa masoko alisema huchochea kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa bidhaa za aina yoyote katika nchi kwani inakadiriwa kuwa asilimia zaidi ya 90 ya mazao na bidhaa zote za ‘horticulture’ zinazozalishwa hapa Zanzibar.
Dk. Mwinyi akipata maelezo kuhusu vifaa vinavyotumika katika tasnia ya hortculture kutoka kwa mmoj ya wadau wa kilimo hicho
Alisema TAHA ni chombo muhimu katika kuendeleza uchumi wa Zanzibar na uwepo wao umekuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya ‘horticulture’ hapa nchini.
Hata hivyo alisema kufunguliwa kwa kituo hicho, kunabainisha nafasi mpya ya Zanzibar katika ukanda wa Afrika ya Mashariki kama miongoni wa vinara wa uzalishaji wa mazao ya bustani na ‘horticulture’.
Akimkaribisha Rais Mwinyi Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Shamata Shaame Khamis, alisema wizara yake ni moja ya taasisi inayopata fursa kutoka kwa wadau wa maendeleo ikiwemo taasisi ya TAHA kuendeleza sekta ya kilimo nchini.
Dk. Mwinyi akipokea zawadi toka kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa TAHA, Jacqueline Mkindi
Mkindi aliongeza kuwa kabla ya kuanzishwa kwa miradi ya kilimo biashara, Zanzibar ilikuwa inaagiza mazao ya matunda na mbogamboga kwa asilimia 80 kutoka maeneo mbali mbali.
Alieleza
kuwa asilimia 42 ya wakulima wa Zanzibar wanalima kilimo cha ‘hortculture’ ambao
wanaendelea na kunufaika na kilimo hicho kupitia TAHA.
Comments
Post a Comment