Simamieni ubora wa bidhaa zinazoingia kuimarisha uzalishaji – Omar

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Omar Said Shaaban, ameitaka Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) kufanikisha malengo iliyojiwekea likiwemo la kudhibiti bidhaa zilizo chini ya viwango kuimarisha uzalishaji wa ndani.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa bodi hiyo katika ofisi za ZBS Maruhubi, Omar aliwataka wajumbe bodi na uongozi kuhakikisha wanashirkiana kukamilisha majukumu yaliyomo katika mpango kazi wa taasisi ikiwemo ujenzi wa ofisi na maabara katika kisiwa cha Pemba.

Aidha aliipongeza bodi hiyo iliyoteuliwa kwa kipindi cha pili kwa kukamilisha ujenzi na upatikanaji wa jengo la ofisi na maabara za kisasa hali iliyoongeza ufanisi wa taasisi kwa wadau wake.

“Sitarajii kuona kunakua na mvutano baina ya bodi na ‘management’ (uongozi) bali natarajia mtaendelea kushirikiana kuleta mafanikio zaidi katika siku za usoni,” alieleza Omar.

Waziri shaaban akisisitiza jambo

Aliwataka wajumbe wa bodi hiyo wanaotoka katika taasisi za serikali na binafsi kutamua kuwa wao ni sehemu ya ZBS hivyo wanapaswa kuwa mabalozi na kusaidia kuondoa changamoto pindi zinapojitokeza.

“Kwa mujibu wa sheria ya ZBS, ukimuacha Mwenyekiti anayetokana na uteuzi wa Mheshimiwa Rais, wajumbe mnatoka katika taasisi za seikali na binafsi hivyo nawaomba msadie ukuaji wa taasisi lakini pia kutatua changamoto zilizopo,” alieleza Waziri huyo.

Aidha aliilekeza taasisi hiyo kukamilisha taratibu za kupata alama ya ithibati wa ubora inayotolewa na Shirika la Viwango la Kimataifa (ISO) ili kuiongezea hadhi na thamani taasisi lakini pia alama ya ubora inayotoa.

Waziri huyo pia aliitaka ZBS kusimiamia udhibiti wa ubora wa bidhaa za nguo, kanga na vitenge zinazoingia nchini ili kukipa uwezo kiwanda cha Basra Textiles wa kushindana.

“Miongoni mwa malalamiko ya kiwanda hiki ni kuwepo kwa bidhaa wanazozalisha katika soko ambazo zipo chini ya kiwango, hivyo nendeni kashughulikieni changamoto hii kukiendeleza kiwanda hiki na vyengine vilivyopo nchini,” alielekeza.

Awali Mwenyekiti wa bodi hiyo Mwanaidi Saleh Abdallah, alieleza kuwa wamejipanga kusimamia majukumu ya taasisi hiyo likiwemo la kukamilisha maandalizi ya mpango kazi pamoja na kuanza ujenzi katika eneo la viwanda Chamanangwe, Pemba.

Mwenyekiti waBodi, Mwanaid Saleh akiwasilisha taarifa

Aliyataja maeneo mengine yatakayosimamiwa na bodi hiyo kuwa ni ujenzi wa eneo la ukaguzi wa magari na kuongeza idadi ya wajasiriamali wanaofikiwa ili kupatiwa alama ya ubora wa bidhaa wanazozalisha ili kuyafikia masoko makubwa.

“Tutahakikisha tunasimamia maandalizi ya mpango mkakati mpya kwani huu uliopo sasa utakamilika mwezi juni lakini pia kuhakikisha tunaongeza ufanisi wa taasisi kwa kuziimarisha maabara zilizopo na kuanzisha nyengine,” alieleza Mwenyekiti huyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa ZBS, Yusuph Majid Nassor, alimshukuru waziri huyo kwa kuiteua tena bodi hiyo kwani ilikua na mashirikiano makubwa na uongozi wa taasisi.

Mkurugenzi Mkuu wa ZBS, Yussufph Majid Nassor, akitoa shukrani na ufafanuzi

Alieleza kuwa katika kipindi cha uhai wa bodi hiyo, ZBS imefanikisha ujenzi wa ofisi na kuanzisha maabara mbali mbali ikiwemo ya bidhaa za petroli na kwamba mchakato wa kuanzisha maabara na ofisi katika eneo la Chamanagwe umeanza.

“Katika bajeti ijayo, tumetenga shilingi milioni 300 kwa ajili ya kuanzisha maabara na ofisi katika eneo la viwanda la Chamanangwe na hivi karibu baadhi ya kazi zikiwemo za maandalizi ya ujenzi huo zitaanza,” alieleza Majid.

Aliongeza kuwa katika kujenga uwezo wa kitaasisi na kuitambulisha kwa jamii, ZBS imelenga kuendeleza majukwaa ya majadiliano na makundi mbali mbali wakiwemo waandishi wa habari kupitia taasisi zao.

Mbali na Mwenyekiti huyo, wajumbe wengine wanaounda bodi hiyo ni Abdallah Mohammed Mmanga anayetokea Jumuiya ya kitaifa ya Wafanyabiashara (ZNCC), Haji Hamid Saleh kutoka Wizara ya Kilimo, Uwagiliaji, Maliasili na Mifugo na Abdullah Rashid Abdullah kutoka Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda.

Baadhi ya wajumbe wa Bodi ya ZBS wakiwa katika picha ya pamoja na Waziri Shaaban

Wengine ni Mkurugenzi wa ZBS, Yusuph Majid Nassor, Khadija Ali Sheha kutoka Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) na mjumbe mmoja kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali.

Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya uongozi ya ZBS wakiwa katika picha na Waziri Shaaban (katikati walioketi) na Mwenyekiti wa bodi, Mwanaidi Saleh (kulia).

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango