Maelfu wamzika Mwakilishi wa Mtambwe

 NA MWANDISHI WETU

MAKAMU wa Pili wa Raiswa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdalluh, ameongoza maelefu ya wananchi na viongozi wa serikali na vyama vya siasa katika maziko ya aliyekua mwakilishi wa jimbo la Mtambwe Pemba, Ali Mohammed (pichani).

Mwakilishi huyo aliyefariki Machi 3, 2023 taarifa za kifo chake zilitangazwa na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid, muda mchache kabla ya kuakhirishwa kwa mkutano wa 10 na kikao cha baraza.

Mbali ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Spika Zubeir, viongozi wengine waliohudhuria maziko hayo ni Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud Othman Masoud Othman, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa chama cha ACT Wazalendo anachotoka mwakilishi huyo.

Akitoa salamu za serikali wakati akiakhirisha mkutano huo, katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani, Hemed alisema huo ni msiba mzito kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wananchi wa Zanzibar na familia huku akimuombea kwa Mwenyezi Mungu kumsamehe makosa yake na kumlaza mahali pema.

Makamu Hemed alisema kutokana na kifo cha Mwakilishi huyo analiahirisha Baraza hadi Mei 10 mwaka huu.

Naye spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid akitoa taarifa ya kifo hicho kwa wajumbe alisema, Mwakilishi Habibu alisibiwa na maradhi Febuari 21 wakati akielekea katika shughuli za baraza, kuanguka hafla na baadae kuwahishwa katika hospitali ya Rufaa Mnazimmoja kwa ajili ya matibabu.

Alisema baadae Mwakilishi huyo alisafirishwa kupelekwa Dar es Salaam kwa matibabu zaidi katika hospitali ya Saifee ya jijini humo.

Awali Spika Zubeir alisema pamoja na juhudi kubwa zilizochukuliwa na madaktari kumhudumia mgonjwa huyo, lakini Mwenyezi Mungu amechukua kiumbe chake.

Aidha alisema kwa kutumia kanuni ya 6(5) ya kanuni za Baraza la Wawakilishi toleo la 2020 ametangaza rasmi kifo cha Mwakilishi huyo na kumuombea kwa Mwenyezi Mungu amsamehe makosa yake.

Wakati huo huo wajumbe wa Baraza hilo waliuaga mwili wa marehemu huyo kabla ya kusafirishwa kupelekwa kisiwani Pemba kwa ajili ya taratibu za mazishi.

Wakizungumza na Zanzibar Leo, baadhi ya wajumbe wa baraza hilo walisema wamepokea kwa simanzi na mshituko mkubwa wa kifo cha marehemu Habibu ambae alikuwa na mchango mkubwa wa kuleta maendeleo ya nchi kupitia chombo hicho cha kutunga sheria.

Walisema pamoja na Mwakilishi huyo kutoka chama cha upinzani, lakini akiwa katika chombo hicho alikuwa anatoa ushirikiano mkubwa katika baraza.  

Mwakilishi wa Jimbo la Nungwi, Abdalla Abass Wadi, alisema marehemu huyo alikuwa mtu wa karibu na hakuwa na majivuno, wala chuki na mfanyakazi mzuri.

Naye Mwakilishi wa Jimbo la Ziwani kisiwani Pemba, Suleiman Makame Ali, alisema marehemu huyo kipindi kifupi tu akiwa katika chombo hicho alikuwa hana ubaguzi na mtu yoyote na hakuwa na chuki wala na ubaguzi wa kisiasa.

“Kwa kweli tulikuwa tunasimama kwa pamoja katika kuisimamia serikali kipindi chote cha uhai wake wakati tukiwa katika chombo hichi pengo lake halitasahaulika,” alisema.

Kwa upande wake Mwakilishi wa nafasi za wanawake Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mwanajuma Kassim Makame, alisema Mwakilishi Habibu alikuwa ni kiongozi hodari na mchapakazi, hana majungu na alikuwa mchangiaji mzuri katika baraza.

Alibainisha kuwa marehemu Habibu alikuwa mtu wa watu na alipewa kipaji na Mwenyezimungu cha kuzungumza na alikuwa hodari katika kuchangia mambo ya maendeleo ya nchi.

Walisema safari hiyo ni ya kila mmoja na kumuombea safari njema, kheri na kumuomba Mwenyezimungu kufutiwa dhambi zake na kaburi lake liwe miongoni mwa bustani za peponi.

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango