Wajasiriamali wanakuza viwango

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema wajasiriamali wanamchango mkubwa katika kukuza viwango nchini na Afrika kwa ujumla.

Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Ali Abdulghulam Hussein alieleza hayo katika maadhimisho ya siku ya viwango Afrika katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil Kikwajuni.

Alisema Rais Mwinyi amekuwa akiwawezesha wajasiamali wadogo kwa kuwawekea fedha ambazo zitawasaidia kuendesha biashara zao kwa ajili ya kujipatia kipato cha kuweza kujikimu.

“Ujasiriamali unawezesha vijana kujiajiri wenyewe na kupata fedha za kujikimu kimaisha lakini pia kukuza pato na uchumi wa nchi ndio maana serikali imekua ikijidhatiti kuweka sera nzuri za elimu na mikakati thabiti ya kulinda na kukuza biashara za wajariamali”, alieleza Naibu Waziri.

Hivyo alisema vyuo vikuu vinaweza kutoa mchango mkubwa katika kukuza tasnia hiyo kwa kufanya tafiti pamoja na kuzalisha wataalamu na wabunifu watakaochochea maendeleo.

Aliwataka wakuu wa vyuo vikuu vya Zanzibar kuendelea kuhamasisha wanafunzi juu ya suala zima la ujasiriamali kwani jambo hilo litawasaidia vijana kujiajiri na kukuza kipato chao.

Sambamba na hayo aliitaka ZBS kubeba jukumu la kuandaa viwango vinavyohitajika na kusimamia utekezaji wake ili kukuza soko la bidhaa za wajasiriamali na kuona bidhaa hizo zinakuwa na ubora unaohitajika.

Alisema serikali inaendelea kuchukua juhudi za kuhakikisha kuwa bidhaa za wajasiriamali zinakuzwa na kupatiwa soko la uhakika huku changamoto wanazokabiliana nazo zinazingatiwa na kutatuliwa.

Akizungumzia mashindano ya insha yanayoandaliwa kila mwaka kwa wanafunzi wa vyuo vikuu yanayosimamiwa na kuendeshwa na Shirika la Viwango Afrika (ARSO) kupitia taasisi za viwango za nchi wanachama, aliipongeza ZBS kwa kutekeleza jukumu hilo kwa Zanzibar.

“Naamini wanafunzi walioshiriki katika mashindano hayo wamejifunza juu ya umuhimu wa viwango na namna vinavyoweza kuimarisha na kukuza sekta ya ujasiriamali barani Afrika”, alisema Abdulghulam.

Naye Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Rashid Ali Salum, alisema serikali inahitaji wataalamu kwa ajili ya kufanya kazi katika tasisi hiyo hivyo suala la elimu lina umuhimu mkubwa.

Hivyo aliitaka ZBS kuhakikisha inachukua jukumu la kutoa elimu zaidi kwa wananchi na wafanyabiashara kuliko adhabu ili kuwawezesha wafanyabiashara kujua umuhimu wa viwango.

“Hatuwezi kuifanya nchi yetu kuwa jaa la bidhaa bandia (feki) lakini tukitoa elimu naamini itasaidia wafanyabiashara wetu kuona na kufahamu umuhimu wa viwango", alisema Salim.

Akitoa maelezo kuhusu maadhimisho hayo, Mkurugenzi Mkuu wa ZBS, Yussuph Majid Nassor, alisema wanachama wa Shirika la Viwango Afrika (ARSO) ikiwemo taasisi hiyo kila mwaka husherehehekea kwa kuitisha shindano la uandishi wa insha.

Alisema wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu Zanzibar huandaa isha kwa kutumia kauli mbiu ya maadhimisho ambapo mchakato huo ulianza mwezi Januari na jumla ya insha 44 zilizoandaliwa na vyuo 13 vya Zanzibar ziliwasilishwa na kupatikana washindi 10.

Mapema Mwenyekiti wa Bodi ya ZBS, Mwanaidi Saleh Abdalla, aliwapongeza vijana walioshiriki katika uandishi wa insha na jambo la fahari ZBS kuendelea kujulikana kwani washiriki wamekuwa wakiongezeka kwani mwaka jana ilikuwa 24 lakini mwaka huu wapo 44.

Aliiomba wizara kuwapa nafasi ya kutoa elimu kwa wanafunzi wa sekondari ili kujua umuhimu wa viwango na kazi zinazofanywa ili kupata vijana wazuri wa baadae watakaosaidia nchi baadae katika sekta ya viwango.

Katika shindano hilo lenye kauli ‘Jukumu la viwango katika kukuza ukuaji wa biashara ndogo ndogo na za kati kwa maendeleo endelevu ya viwanda na Uchumi Afrika', mwanafunzi Maryam rajab Othman kutoka chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kampasi ya Karume aliibuka mshindi wa kwanza.

Aidha Rahma Gharib Mohamed kutoka Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) kampasi ya Tunguu alishika nafasi ya pili na Hafidh Said Nassor wa SUZA kampasi ya Vuga aliibuka mshindi wa tatu ambao walikabidhiwa zawadi laptop, kishikwambi, vyeti pamoja na fedha taslim.

PICHA:

NAIBU Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ali Abdulghulam Hussein, (wa pili kulia) akikabidhi zawadi ya mshindi wa kwanza wa shindano la uandishi wa insha kwa mwanafunzi wa chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kampasi ya Karume Zanzibar, Mariam Rajab Othman, kuadhimisha Siku ya Viwango Afrika.

MKURUGENZI Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS), Yussuph Majid Nassor, akitoa maelezo ya wakati wa maadhimisho ya Siku ya Viwango Afrika yaliyofanyika jana katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakili Kikwajuni jijini Zanzibar.


Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango