Dk. Mwinyi aongoza viongozi, wananchi kumuombea mzee Karume

 

NA MWANDISHI WETU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi jana amewaongoza wananchi wa Zanzibar, katika dua maalum ya kumbukumbu ya kifo cha Rais wa Kwanza wa Zanzibar Hayati Abeid Amani Karume aliyefariki dunia Aprili 7 mwaka 1972.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, akiweka shada la maua katika kaburi la marehemu mzee karume.

Dua hiyo iliyoanza majira ya saa 3:00 asubuhi ilifanyika katika Ofisi Kuu za Chama cha Mapinduzi (CCM) Kisiwandui Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali kutoka serikali zote mbili na viongozi wa chama cha Mapinduzi.

Mara baada ya kumalizika kwa kisomo cha dua, Dk.  Mwinyi alianza kuweka shada ya maua katika kaburi la mzee Karume, akifuatiwa Makamu wa Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Mpango, wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama, mabalozi na Ali Abeid Amani Karume akiwakilisha familia. 


MTOTO wa marehemu Rais wa kwanza wa Zanzibar marehemu mzee karume, ambaye pia ni Rais mstaafu wa zanzibar awamu ya sita Amani Abeid Karume (wa pilikushoto) akiitikia dua pamoja na viongozi wengine katika kaburi la marehemu mzee Karume.

Wakimzungumzia hayati Karume baada ya dua hiyo viongozi mbalimbali walisema marehemu Karume alikuwa ni kiongozi muandalifu na mpenda maendeleo ambae aliipatia heshima Zanzibar. 

Akizungumza na gazeti hili, Balozi Ali Karume alisema miaka 51 imepita tokea mzee Karume alipouawa, lakini wakati wa uhai wake alifanya mambo mengi ambayo yamebakia kama kielelezo cha matunda ya mapinduzi ikiwemo kuondoa ubaguzi wa aina yeyote.

“Mzee Karume atakumbukwa kwa mambo mengi ikiwemo kuondoa ukabila na kuwaweka watu wote sawa mambo ambayo yanatakiwa kuendelezwa kwa nguvu zote.

Mnadhimu Mkuu wa JWTZ Luteni Jenerali, Salum Haji Othman, akiweka Shada la maua katika Kaburi la Rais  wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume

Kwa upande wake Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar, Khamis Mbeto Khamis, alisema mzee Karume aliongoza Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 ambapo viongozi wanapaswa kuiga mambo mazuri aliyoyafanya wakati wa uhai wake. 

“Tunaadhimisha kuwakumbuka wazalendo waliojitolea maisha yao kupigania uhuru nchi yetu. Tunaipongeza na kuishukuru serikali kuandaa utaratibu mzuri wa kuanzia kwenda kuwasomea dua waasisi wengine ambapo Aprili 7 kila mwaka ndio siku maalum ya kumuombea dua mzee Karume”, alisema. 

Balozi wa China Nchini Tanzania  Shang Shisceng akitoa heshima baada ya kuweka shada la maua katika Kaburi la Rais  wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume

Kwa upande wake Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mgeni Hassan Juma, alisema wananchi wa Zanzibar wana kila sababu ya kumkumbuka na kumuenzi Mzee Karume kutokana na uongozi wake bora.

Alisema wazanzibari hivi sasa wanatembea kifua mbele na wapo huru kufanya maamuzi yao wenyewe, wanajitawala wenyewe kutokana na wakati wa utawala wa mzee Karume aliweka misingi thabiti kiutawala. 

Baadhi ya waumini na wananchi wa Zanzibar wakifuatilia dua ya kumuombea Rais  wa kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume

Hata hivyo, alisema Mzee Karume ni kiongozi wa mfano kutokana na mambo mengi aliyoyafanya na mpaka leo yanaishi hali inayoonesha wanaishi nae katika dunia ya sasa. 

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Dk. Saada Mkuya Salum, alisema kila kiongozi ana wajibu wa kufuata misingi aliyoweka marehemu Karume ili kuyafikia malengo kuiinua Zanzibar kimaendeleo. 

Kwa upande wake, waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Masoud Ali Mohammed, alisema kuna mambo mengi ya kujifunza kila unapouangalia uongozi wa mzee Karume.


MJANE wa  Rais  wa kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, Fatma Karume (wa tatu toka kulia) akijumuika na viongozi wengine akiwemo mke wa rais wa Zanzibar mama Mariam Mwinyi (wa pili toka kulia) katika dua ya kumuombea mzee Karume.

Kisomo cha kumuombea marehemu mzee Karume kilihudhuriwa na viongozi mbalimbali, wananchi na wanafamilia akiwemo mama Fatma Karume, Dk. Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Mpango, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla na Rais Mstaafu wa Zanzibar wa awamu ya sita Dk. Amani Abeid Karume.

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango