Serikali yaahidi msukumo uzalishaji mazao ya nyuki
NA MWANDISHI WETU
WIZARA
ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda imeeleza kuwa itaendelea kutoa msukumo kwa
wafugaji wa nyuki na wazalishaji wa mazao ya nyuki ili kuimarisha uchumi wao na
na tija kwenye kilimo.
Hayo yameelezwa na
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Ali Khamis Juma, alipokua akizungumza katika
maadhimisho ya Siku ya Nyuki Dulinani yaliyofanyika Kitogani, mkoa wa Kusini
Unguja.
Alieleza kuwa
kutokana na faida zinazopatikana kwenye ufugaji wa nyuki, ipo haja kwa Wizara ya
Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo kuweka mkazo wa kuiimarisha sekta hiyo
ili isaidie ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
“Kama mlivyoeleza
hapa, nyuki ana faida nyingi kiuchumi na kijamii hivyo wakati wizara mnaendelea
na mapitio ya sera ya misitu, mnaweza kutunga kanuni za misitu na nyuki ili
kulinda makundi ya nyuki yaliyoanza kupotea”, alieleza Juma.
Aidha aliwataka
wafugaji hao kufuata maelekezo ya wataalamu sambamba na kulinda uoto wa asili
ili kuzalisha bidhaa zitakazotosheleza soko la ndani na nje ya nchi.
“Niwatie moyo na
kuwahakikishia kwamba mtakapozalisha bidhaa zinazotokana na nyuki, wizara yetu
itawapatia msaada wa kiufundi na kitaalamu ikiwemo kuwapatia alama ya ithibati
ubora ili kulifikia soko la kimataifa”, alieleza Katibu Mkuu huyo.
Aidha aliipongeza wizara
ya kilimo na wadau mbali mbali kwa juhudi inazochukua kuhakikisha sekta ya
nyuki inawanufaisha wananchi kwa kuwajengea uwezo wafugaji nyuki wa Unguja na
Pemba.
Akimkaribisha
Katibu huyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo,
Seif Shaaban Mwinyi, aliwahimiza vijana kujikita katika shughuli za ufugaji
nyuki na uhifadhi misitu.
Alieleza kuwa
kufanya hivyo kutapunguza tatizo la ajira, kulinda afya zao na kuwaahidi
wanachama wa jumuiya za wafugaji nyuki kwamba wizara itaendeleza mikakati ya
kuziimarisha ili ziendelee kuwanufaisha wengi.
Nae Mkurugenzi wa Idara
ya Misitu, Said Juma Ali, alieleza kuwa sekta ya nyuki na uzalishaji wa asali
na mazao mengine ya nyuki imeendelaa kuimarika kiasi cha kufikia wafugaji 1,531
waliosajiliwa na kutambulika rasmi.
Alisema idadi hiyo
inaweza kuongezeka na kuongeza uzalishaji wa asali na kufikia malengo
yaliyowekwa na ilani ya uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ya Zanzibar kuzalisha
tani 25 ifikapo mwaka 2025.
“Ili kufikia hatua
hiyo wizara imeanza mapitio ya sera ya misitu, kuimarisha mkakati wa elimu ya
ufugaji nyuki lakini pia kuandaa rasimu ya sera na kutangaza misitu ya hifadhi
ya nyuki ili kuimarisha maisha yao”, alieleza Juma.
Akisoma risala kwa
niaba ya wafugaji wenzake, Mtumwa Rashid Khamis, alileza kuwa maadhimisho hayo
ni ya saba toka siku hiyo ilipotangazwa na umoja wa mataifa kwa lengo la
kuimarisha ulinzi wa nyuki ili kusaidia ukuaji wa uchumi na maisha.
Alieleza kuwa licha
ya faida zinazopatikana kupitia nyuki bado ufugaji wake unakabiliwa na
changamoto kadhaa ikiwemo ya uharibifu wa misitu na matumizi ya dawa na
viatilifu kwenye kilimo.
Alizitaja
changamoto nyengijne kuwa ni mabadiliko ya tabia nchi, ughali wa vifaa vya
kufugia na kuvunia asali na mazao mengine ya nyuki kama vile chavuo, sumu ya
nyuki, nta, maziwa ya nyuki na gundi la nyuki ambazo zina thamani kubwa.
Siku ya nyuki
duniani huadhimishwa kila ifikapo Mei 20 ya kila mwaka, ambapo Jumuiya ya
Wafugaji Nyuki Zanzibar (ZABA), Jumuiya ya Ufugaji Nyuki Pemba (PEBA) ziliiadhimisha
siku hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya kilimo kupitia Idara ya Misitu kwa
mafunzo ya ufugaji na kuzindua vifaa vya kuvunia mazao ya nyuki na utalii wa
nyuki (bee tour).
Comments
Post a Comment