Wanafunzi MCC, MSJ watakiwa kusoma kwa bidii

NA ASYA HASSAN

WANAFUNZI wanaosomea fani ya habari katika chuo cha Mwenge Community Center (MCC) na Morogoro School of Journalis (MSJ) wametakiwa kusoma kwa bidii ili kuwa wataalamu wazuri wa fani ya habari wanapomaliza masomo yao.



Mwenyekiti wa KLABU ya Waandishi ya Habari Zanzibar (ZPC), Abdallah Abdulrahman Mfaume, alitoa rai hiyo alipokuwa akizungumza na wafunzi hao chuoni kwao Amani, ikiwani mwendelezo wa shughuli za maadhimisho ya miaka 30 Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani iliyoadhimishwa Mei 3, mwaka huu.

Alisema hatua hiyo itawasaidia kuwa ujasiri katika kutekeleza vyema majukumu ya kuisemea jamii kwaniu tasnia hiyo ni muhimu katika kuchochea maendeleo na ustawi wa jamii.

“Leo mpo chuoni lakini mtakapotoka hapa mtakwenda kuitumikia jamii hivyo kuna umuhimu kwenu kujikita katika masomo ili maarfa mnayoyapa mkayatumie kuimarisha ustawi wa jamii na maendeleo ya nchi”, alieleza Mfaume.

Sambamba na hayo aliwataka waandishi wa habari hapa nchini kuacha mihemko wanapotekeleza majukumu yao badala yake kuzingatia misingi na maadili ya tasnia hiyo ili kuepuka kuleta taharuki nchini lakini pia kufanya kazi kwa ufanisi.

Nae Mkufunzi wa chuo hicho, Omar Abdalla Juma, alipongeza uamuzi wa klabu hiyo kwenda katika chuo hicho na kukutana na wanafunzi kuwakumbusha wajibu wao na kuwaonesha mahali wanapoweza kufikia pindi wanapomaliza masomo yao.

“Hatua hii imeonesha ni namna gani jumuiya hii inathamini taasisi zinazotoa taaluma ya uandishi kama hii ambayo imetoa watendaji wengi wa vyombo vya habari na fani nyengine zinazofundishwa hapa”, alieleza Omar.

Aidha aliwaomba wanafunzi hao na waandishi wa habari waliopo kazini kuendelea kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili na miongozo ili wazidi kutoa sifa njema ya chuo hicho na kada ya uandishi wa Habari.

Nae Kaimu Mkuu wa chuo cha MSJ, Mohamed Ali Mohamed, aliwahimiza wanafunzi hao kuthamini juhudi zinazochukuliwa na wadau mbali mbali kuiimarisha kada hiyo hivyo wanapaswa kuzingatia nidhamu na maadili wanapopata nafasi ya kwenda kuitumikia jamii.

Hata hivyo aliwashauri kujiungana klabu hiyo ili wazidi kupata uelewa na uwezo wa kujiamini wanapokuwa katika majukumu yao ya kazi na kuishukuru ZPC kwa msaada wa vitabu na majakreti ya usalama walivyovitoa kwa chuo hicho.

Mapema akielezesa madhumuni ya mkutano huo, Katibu Mkuu wa ZPC, Mwinyimvua Abdi Nzukwi, alieleza kuwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Habari ambapo klabu hiyo iliona ni vyema kukutana na wanafunzi wa vyuo vya Habari ili kuwajegea uwezo wa kujieleza kama moja ya haki zinazotambulika kikatiba.

“Mhadhara huu unalenga kuibua mijadala juu ya haki na uhuru wa kujieleza lakini pia kuangalia nafasi za asasi za kihabari zinazvyoweza kukuza Uhuru wa Habari na taaluma ya uandishi wa Habari nchini”, alieleza.

Wakizungumza katika mhadhara huo, baadhi ya wanafunzi wanaosoma chuoni hapo waliishukuru ZPC kwa kwenda kuwapatia taaluma hiyo na kuwaonesha njia ya kutekeleza majukumu yao pale watapokuwa wamemaliza masomo yao.

Akifunga mhadhara huo, Makamu Mwenyekiti wa Klabu hiyo, Tabia Makame Mohammed, aliwataka wanafunzi hao kuvunja ukimya dhidi ya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia vinavyofanywa na baadhi ya watendaji wa vyombo vya Habari.

Alieleza kuwa kuna malalamiko ya wanafunzi kufanyiwa vitendo hivyo wanapokwenda kwenye mazoezi ya vitendo katika vyombo vya habari, jambo ambalo ni kinyume na maadili ya uandishi wa habari na haki za binaadamu.

Mbali na mkutano huo ZPC ilikabidhi vitabu vinavyohusiana na uandishi wa habari  kwa lengo la kuimarisha maktaba ya chuo hicho kuwasaidia wanafunzi kuongeza maarifa lakini pia makoti ya usalama kwa ajili ya waandishi wa redio ya chuo hicho.

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango