ZBS yanasa nyaya ‘feki’ za umeme
TAASISI
ya Viwango Zanzibar (ZBS) imezuia matumizi na usambazaji wa nyaya za umeme (PVC Cable) zenye jina la Kili Cable na namba ya utambulisho TP/EEL/18/2023 baada ya kugundulika kuwa zipo chini ya viwango.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari katika ofisi za taasisi hiyo Maruhubi, Mkurugenzi Mkuu wa ZBS, Yussuph Majid Nassor, ameeleza kuwa mbali ya kuwa chini ya kiwango, pia mtengenezaji amefoji jina la kibiashara la bidhaa hiyo.
Majid ameeleza kuwa hatua hiyo imekuja baada ya kupata taarifa za kuwepo kwa bidhaa hiyo sokoni zilizoingizwa nchini na mfanyabiashara
asiyefahamika jambo ambalo ni kinyume na sheria.
Amesema kuwa baada
ya kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema, ZBS ilichukua sampuli za bidhaa
hiyo na kuifanyia uchunguzi wa kimaabara na kugundulika kutokidhi viwango
vilivyowekwa.
“Tulipochukua sampuli za waya hizo na kuzipima kwenye mabara zetu, ripoti ya upimaji wa sampuli hizo imenakiliwa kuwa bidhaa hii imefeli katika kipengele cha ‘sheath’ (unene wa waya
wa nje)”, ameeleza Majid.
Amefafanua kuwa waya
huo ulitakiwa kuwa na unene wa 1.5mm2 kulingana na matakwa ya kiwango cha ZBS lakini
uligundulika kuwa na 1.05mm2 jambo linaloweza kuleta madhara kwa
watumiaji.
Hivyo aliwaomba wananchi kuendelea kushirikiana na taasisi hiyo kwa kutoa taarifa wanapozigundua bidhaa zenye utambulisho huo huku akilishukuru jeshi la polisi na Tume ya Ushindani Halali wa Biashara Zanzibar kwa kushiriki operesheni ya kuondoa bidhaa hizo madukani.
Majid ameeleza kuwa mbali ya hatua zilizochukuliwa, wamelifikisha swala hilo polisi na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu uchumi kwa hatua zaidi kufuatia kunakiliwa kwa bidhaa hiyo jambo ambalo ni kosa kisheria.
“Kwa mujibu wa sheria
ya viwango namba 1 ya 2011 pamoja na mambo mengine, ZBS imepewa jukumu la
kulinda ubora wa bidhaa zinazoingizwa au kuzalishwa nchini lakini pia kulinda viwanda
na wazalishaji halali ndio maana swala hili tumelifikisha huko ili kulinda haki
za kampuni ya AfriCab”, ameeleza Mkurugenzi huyo.
Aidha amesema ZBS
inaendelea na uchunguzi juu ya bidhaa hizo na taarifa za kuwepo kwa mchele
uliioamriwa kurudishwa ulipotoka baada ya kukosa viwango katika masoko ya
Zanzibar na kwamba hatua zitachukuliwa kwa wahusika.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, bidhaa hizo zimegunduliwa
kuwepo sokoni mapema mwezi huu kabla ya Mei 11, mwaka huu taasisi hiyo kufanya
operesheni ya kuziondoa na kisha kubaini kuwa hazikukaguliwa kabla wala baada hazijaingia nchini kupitia mifumo ya ukaguzi ya taasisi hiyo.
Comments
Post a Comment