Dk. Mwinyi abainisha kipaumbele cha SMZ

NA MWANDISHI WETU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussain Ali Mwinyi, amesema sekta ya elimu ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mujibu wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2020 - 2025.

 Dk. Mwinyi aliyasema hayo alipoweka jiwe la msingi wa ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Kampasi ya Pemba eneo la Mtima shehia ya Pujini, Wilaya ya Chake Chake, mkoa wa Kusini Pemba.

Aliupongeza uongozi wa chuo hicho kwa kuona umuhimu wa kufungua Kampasi hiyo kisiwani Pemba ikiwa ni sehemu sahihi ya kusogeza huduma za jamii ikiwemo kutanua fursa zaidi za elimu kwa watu wa Pemba na Watanzania kwa ujumla.

Aidha Dk. Mwinyi alisema serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na Chuo hicho kwa kutoa mafunzo mbali mbali zikiwemo ngazi za Astashahada, Stashahada, Shahada na Shahada ya Uzamili.

Alisema, pamoja na mafunzo ya ngazi hizo za kielimu, Chuo pia kimekuwa na mchango mkubwa kwa kutoa mafunzo ya Uongozi, Maadili na Uzalendo kwa wanachuo na watumishi mbalimbali wa umma ambao wanasaidia kutekeleza majukumu yao ndani ya Serikali. 

Alieleza chuo hicho kina uzoefu wa kutoa wahitimu walioiva, wenye uadilifu, uzalendo na weledi wa hali ya juu, ambazo ni nyenzo muhimu kwa mtumishi yoyote anayepewa dhamana ya utumishi wa Umma. 

Pia, alikipongeza chuo hicho kwa kutekeleza mipango ya serikali kwa vitendo hasa kufuata maelekezo mbali mbali ya Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya Serikali ya Muungano na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa kuongeza udahili wa wanafunzi wengi na ujenzi wa miundombinu ya taasisi za elimu.

Hata hivyo, Dk. Mwinyi aliwahimiza wanafunzi wa chuo hicho kusoma kwa bidii na nidhamu ili kutimiza malengo yao pamoja na kuhakikisha wanafuata sheria za nchi, kanuni na taratibu za Chuo muda wote wanapokuwa chuoni. 

Naye, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ali Abdulgulam Hussein, alisema serikali ina nia ya kubadilisha sheria ili wanafunzi wa diploma wapate fursa ya mikopo nao wajiunge na vyuo vyengine vikuu pia aliishukuru Serikali kwa kuwaongezea bajeti hasa kwenye Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ya Zanzibar, hali aliyoieleza itawapa uwezo wanafunzi wengi kuhudhuria vyuoni.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkuu wa mkoa wa Kusini Pemba, Mattar Zahor Masoud, alisema alisifu kazi inayofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya Elimu nchini aidha, alieleza Mkoa wa Kusini Pemba kwa mwaka huu wa 2023 umetoa matokea mazuri kwa asilimia 99.9 ya wanafunzi wote waliofanya mitihani ya kidato cha sita, hivyo aliwaondolea hofu Chuo hicho kwa kukosa wanafunzi wakujiunga. 

Mapema  Mwenyekiti wa Bodi ya chuo hicho, Steven Masato Wasira, aliishikuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano wanaoutoa kwa chuo hicho, hata kwa kamapasi yao ya Karume kwa kueleza kuwa SMZ imekua msaada mkubwa hasa wanapofanya shughuli za chuo zinazohusisha masuala ya serikali na matukio ya kitaifa.

Alisema, dhamira ya chuo hicho ni kutoa elimu ya juu iliyobora, pia kutoa nafasi kwa walimu kujiongezea maarifa kupitia viwango vya juu zaidi vya elimu.

Comments

Popular posts from this blog

Balozi Mpanda ahimiza ubunifu uhifadhi wa mazingira

Vodacom yawapa uhakika wa matibabu mama, watoto wachanga