Dkt. Mwinyi ahimiza ubunifu huduma za bima ZIC
NA MWANDISHI WETU
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi (wa pili toka kulia) amezindua huduma ya bima inayofuata misingi ya dini ya Kiislamu (Takaful) inayotolewa na Shirika la Bima Zanzibar (ZIC) na kulipongeza shirika hilo kwa ubunifu wa huduma hiyo hiyo itakayowavutia wananchi waliokua wakiepuka huduma za bima kwa mitazamo ya imani ya kidini.
Uzinduzi huo ulifanyika jijini Zanzibar
Julai 5, mwaka huu ambapo huduma hiyo itakuwa inatolewa na ZIC kupitia kampuni
yake tanzu inayofahamika kama ZIC Takaful ambapo dkt. Mwinyi alisisitiza azma
ya serikali ya mapinduzi Zanzibar kuhakikisha huduma za bima zinawafikia
wananchi wote bila ya vikwazo vya kiimani bali matakwa yao.
Dkt. Mwinyi akizungumza na watendaji wa ZIC na wadau mbali mbali
wa huduma hiyo wakiwemo viongozi wa serikali, dini, wadau wa bima, taasisi za
fedha na wananchi, amesema huduma hiyo imekua ikitolewa maeneo mbali mbali
ulimwenguni hivyo itaongeza sifa za uwekezaji nchini.
“Kwa muda mrefu sasa huduma ya Takaful imekuwa ikitumiwa katika
nchi mbali mbali za barani Afrika, Ulaya na Asia ili kutoa fursa kwa biashara
ambazo zinafuata misingi ya Kiislamu. Ujio wa huduma hii hapa nchini
utatusaidia pia kuwavutia wawekezaji wanaoamini katika imani hii hatua ambayo
ni muhimu kwa maendeleo ya shirika na taifa kwa ujumla’’ amesema.
Alibainisha kuwa huduma hiyo inatarajiwa kuwa kiungo muhimu
katika ukuaji wa huduma za fedha zinazofuata misingi ya kiislamu kwani hutoa
fursa kwa mabenki ambayo tayari yanaendeshwa kwa misingi hiyo, kuweza kutoa
huduma za bima jambo ambalo halikuwezekana kabla ya uanzishwaji wa Takaful.
Aidha Dkt. Mwinyi alibainisha kuwa lengo la serikali ni kuona
kamba wananchi wote bila kuathiri imani zao za kidini wanafikiwa na huduma
mbalimbali zi kiuchumi zinazotolewa na taasisi mbalimbali huku akipongeza
baadhi ya mashirika na taasisi likiwemo Shirika la Bima Zanzibar kwa namna
linavyotafsiri vema nia hiyo ya serikali.
Awali akizungumza kwenye uzinduzi huo Naibu Waziri wa Fedha na
Mipango Zanzibar, Ali Suleiman Ameir, amesema ujanzishwaji wa huduma ya Takaful
unakwenda sambamba na jitihada za serikali za kuimarisha sekta ya bima na
kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi hatua ambayo ina manufaa makubwa kwa
serikali, wananchi na taifa kwa ujumla.
“Kwa upande wa serikali, huduma ya Takaful itasaidia kuongeza
mapato ya serikali kupitia kodi na tozo zinazopatikana kutokana na shughuli za
bima. Hii itachangia kuimarisha uwezo wa serikali wa kutoa huduma muhimu kwa
wananchi na kutekeleza miradi ya maendeleo. Tunawapongeza sana ZIC kwa hatua
hii muhimu”, alisema.
Alisema serikali imejipanga
kuhakikisha huduma ya Takaful inaendeshwa kwa ufanisi mkubwa na tayari imeanzisha
mifumo madhubuti ya udhibiti na ukaguzi ili kuhakikisha uwazi, uwajibikaji, na
uaminifu katika shughuli za bima ikiwemo huduma hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZIC, Arafat Haji alisema
hatua hiyo muendelezo wa mkakati wa msingi wa shirika hilo unaolenga
kuhakikisha huduma zake zinawafikia watu wote lengo likiwa ni kuimarisha
upatikanaji wa huduma za bima kwa wananchi na hivyo kuongeza kasi ya ukuaji
wake na ule wa taifa kwa ujumla.
“Tunaamini kwamba huduma hii Takaful inakwenda kutujengea
taswira bora zaidi mbele ya wadau wetu wote imani ambayo tunaamini itatujenga
zaidi kibiashara na hivyo kutuhakikishia uwezo wetu katika kulinda miradi,
biashara na mali za wawekezaji wetu huku pia tukiongeza ajira kwa wananchi”, amesema
Arafat.
Mkurugenzi Arafat ameongeza kuwa, huduma ya Takaful itaongeza
kasi, nguvu ya ukuaji na kuunga mkono jitihada mbali mbali zinazoendelea
kufanywa na taasisi za kifedha nchini ambazo zinabuni huduma zinazoendana na
misingi ya imani ya Kiislamu.
Naye Kamishna wa Bima Dkt. Baghayo Saqware alisema kwa
sasa soko la bima nchini linahudumia asilimia 15 hadi 20 tu ya wananchi wote
hivyo ubunifu unaolenga kuongeza watumiaji wa huduma hiyo ni muhimu kwa kuwa ni
adhma ya serikali kuwa na mfumo jumuishi wa utoaji wa huduma hiyo muhimu
kiuchumi.
“Sekta ya Bima ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja
mmoja, taasisi na serikali kwa ujumla na hiyo ndio sababu tunalishukuru Shirika
la Bima Zanzibar kwa hatua hii, inayolifanya shirika hili kuwa la kwanza nchini
kutoa huduma ya bima ya Takaful”, alieleza Kamishna huyo.
Huduma ya Takaful inazingatia misingi na maadili ya dini ya Kiislamu ikiwemo kutohusisha riba, kamari, huku ikipinga uwekezaji katika biashara zinazokwenda kinyume na misingi ya dini hiyo.
Comments
Post a Comment