Maonesho ya nane nane kuinua kilimo Zanzibar - Shamata

NA MWANDISHI WETU

WIZARA ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Misitu imeeleza kuwa itaendelea kutumia mbinu mbali mbali kushajihisha jamii hasa vijana na wanawake kushiriki kwenye kilimo ili kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira nchini.

Waziri wa wizara hiyo, Shamata Shaame Khamis, alieleza hayo jana huko Dole, wilaya ya Magharibi ‘A’ Unguja, alipokua akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maonesho ya Siku ya Wakulima (nane nane) yatakayofanyika katika viwanja vya Dole Kizimbani mwezi ujao.

Shamata alieleza kuwa maoenesho hayo limekua jukwaa muhimu kwa wakulima na wadau wa sekta ya kilimo kupata taarifa, maarifa na ujuzi unaochochea ushiriki wao kwenye kilimo lakini pia kuongeza uzalishaji wa mazao hivyo kuifanya nchi kuwa na uhakika wa chakula.

“Kupitia maonesho wadau watajifunza mbinu na teknolojia mpya za kuongeza uzalishaji lakini pia kujiunga na shughuli za kilimo na kuongeza mnyororo wa thamani ya mazao yanayozalishwa hivyo kukifanya kilimo kuendelea kuwa na tija kwa maisha ya watu na uchumi wa nchi”, alieleza Shamata.

Aidha alieleza kauli mbiu ya maonesho ya mwaka huu ni ‘Vijana na wanawake ni msingi imara wa mifumo endelevu ya chakula’ ambayo inalenga kutambua mchango wa vijana na wanawake katika kilimo.

Aidha aliongeza kuwa ujumbe huo unalenga kutoa fursa zaidi kwa vijana na wanawake kujiekeza katika sekta ya kilimo kwa manufaa yao wenyewe, familia zao na kwa taifa kwa jumla kwa kuchochea ukuaji wa uchumi na kupunguza utegemezi.

Akizungumzia mikakati ya wizara hiyo katika kuinua kilimo nchini, Shamata alieleza kuwa serikali imeongeza bajerti ya kilimo ambayo kwa mwaka 2023/2024 imeongezeka hadi kufikia shilingi 98.7 bilioni kutoka shilingi 53.5 bilioni ya mwaka 2022/2023.

“Wizara pia inalenga kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji ikiwemo ujenzi wa Hekta 300 katika bonde la Cheju ‘B’ na ujenzi wa misingi ya ndani kwa kiwango cha saruji yenye urefu wa kilomita 47.7 kwenye mabonde yote mapya ya umwagiliaji ya Kinyasini, Cheju, Mlemele, Kibokwa, Chaani  na Kilombero”, alieleza Shamata.

Alieleza mkakati mwengine kuwa ni kuongeza upatikanaji vifaa na nyenzo za kilimo zitakazowavutia vijana na wanawake kushiriki kwenye shughuli za kilimo, kuongeza idadi ya watalii katika hifadhi hadi kufikia watalii 100,000 kutoka 64,000 wa mwaka 2022/2023, kuimarisha miundombinu ya  mifugo na kuimarisha mnyororo wa thamani katika ufugaji wa nyuki.

Akizungumzia umuhimu wa sekta hiyo kwenye uchumi, shamata alieleza kuwa kwa kipindi kirefu kilimo kimekua kikichangia zaidi ya asilimia 20 ya pato la taifa na kuajiri karibu asilimia 40 ya Wazanzibari na zaidi ya asilimia 70 wamejiajiri kwa njia moja na nyengine kutegemea sekta ya kilimo kwa ustawi wa maisha yao ya kila siku.

“Sekta ya kilimo ni uhai ni afya, ni maisha ni uti wa mgongo na ni muhimili muhimu katika kuimarisha uhakika, usalama na mifumo ya chakula kwa ujumla”, alieleza Waziri huyo.

Awali Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Seif Shaaban Mwinyi, alieleza kuwa maandalizi ya maonesho hayo yanaendelea vyema kupitia kamati ya maandalizi inayoshirikisha watendaji wa wizara na taasisi nyengine.

Alieleza kuwa maonesho hayo yanayofanyika kwa mara ya tano toka yalipoasisiwa, yamesaidia kuwaweka pamoja wadau wa sekta ya kilimo kuzitambua changamoto zinazowakabili na kuzipatia ufumbuzi.

Hata hivyo alitoa wioto kwa wadau wa kilimo ndani na nje ya Zanzibar kuendelea kujitokeza kuchukua fomu za ushiriki na kusaidia ufanikishaji wa maonesho hayo ambayo alisema yanamgusa kila mmoja miongoni mwa jamii.

Maonesho ya Siku ya Wakulima (nane nane) yatafanyika kwa mara ya tano kuanzia Agosti 1 hadi 10, mwaka huu yanatarajiwa kufunguliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ambapo zaidi ya taasisi 200 za serikali na binafsi zinatarajiwa kushiriki.

Comments

Popular posts from this blog

Balozi Mpanda ahimiza ubunifu uhifadhi wa mazingira

Vodacom yawapa uhakika wa matibabu mama, watoto wachanga