SMZ kujenga mahakama, miundombinu huduma za jamii

NA MWANDISHI MAALUM, IKULU

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema itazijenga upya mahakama zote za Zanzibar a kupitia bajeti ya mwaka wa Fedha, 2023/2024.

Aidha, imeeleza dhamira yake ya kukamilisha miradi yote ya maendeleo ndani ya kipindi cha mwaka mmoja kwa sekta zote zikiwemo, afya, elimu, maji safi, miundombinu ya barabara, ujenzi wa ofisi  za serikali pamoja na sekta ya michezo.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi aliyasema hayo aliposhuhudia utiaji wa saini  mkopo wa shilingi bilioni 470 zilizotolewa na benki ya NBC na benki ya NMB kwa upannde mmoja na Wizara ya Nchini Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango hafla iliyofanyika Ikulu, Zanzibar.

Dk. Mwinyi amesema hii ni mara ya kwanza kwa SMZ kukopa Fedha kutoka benki za ndani na kuahidi kuzirejesha fedha hizo kwa kipindi kifupi kwani Serikali inauwezo wa kufanya hivyo na sasa inaakiba ya kurejesha gharama nusu za mkopo huo.

Dk. Mwinyi alisema Fedha hizo zimekusudiwa kukamilisha miradi yote ya maendeleo ndani ya kipindi cha mwaka mmoja wa Fedha 2023/2024.

Alisema, awali serikali ilitumia Dola za Marekani milioni 100 sawa na shilingi bilioni 230 za Tanzania kwa ajili ya miradi mbali mbali ya maendeleokwa fedha za ahuweni ya UVIKO 19.

Alisema, kupitia Fedha hizo, Serikali ilifanikiwa kujenga skuli za ghorofa na hospitali za wilaya kwa Wilaya zote za Unguja na Pemba.

Dk. Mwinyi aliishukuru benki za NBC na NMB kwa ushirikiano wao wanaoutoa kwa kuungamkono juhudi za Serikali za kuwainarishia wananchi maendeleo.

Aidha, alizitaka benki hizo kuongeza kima kikubwa zaidi kwa kuikopesha Serikali mara baada ya kurejesha mkopo huo.

Alieleza dhamira ya Serikali  kuondosha tatizo la maji Safi na salama kwa maeneo yote ya Unguja na Pemba hasa kwa mikoa ya Kusini na Kaskazini Pemba ambako alieleza kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji safi.

Mapema akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Sada Mkuya Salum amesema fedha hizo zitatumika kwa mujibu wa Sheria na taratibu zilizowekwa ili kukamailisha miradi ya maendeleo kwa wakati.

Waliotia saini kwenye hafla hiyo ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dk. Juma Malik Akil, Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya NBC, Theobald Sabi na Mkurugenzi wa fedha za ndani wa benki ya NMB, Juma Kimori.

Comments

  1. Great hii itasaidia kukuza ustawi na maendeleo ya nchi na watu wake lkn upatikanaji wa haki na usawa kwenye jamii

    ReplyDelete

Post a Comment

Popular posts from this blog

Balozi Mpanda ahimiza ubunifu uhifadhi wa mazingira

Vodacom yawapa uhakika wa matibabu mama, watoto wachanga