Toeni taarifa za madhila mnayofanyiwa kazini – Simbaya

NA MWANDISHI WETU


MKURUGENZI Mtendaji wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Kenneth Simbaya (wa pili kushoto aliyeshikana mikono na Katibu wa KGPC - Mwajabu Hoza)  amewahimiza waandishi wa Habari kutoa taarifa za madhila wanayofanyiwa wanapokua kazini ili hatua zichukuliwe.

Simbaya alitoa wito huo mkoani Kigoma alipokua akizingumza na waandishi wa habari wanachama wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani humo (KGPC), alipofika kujitambulisha kwa wanachama na kueleza mipango ya utekelezaji wa mpango wa mkakati wa UTPC wenye kaulimbiu ya ‘Kutoka kwenye ubora kwenda kwenye ukubwa (Moving from good to great).

Mkurugenzi huyo aliyembatana na Ofisa Programu, Mafunzo, Utafiti na Machapisho, Victor Maleko, alisema hatua hiyo itapunguza vitendo hivyo vinavyopunguza uhuru wa vyombo vya habari nchini.

MKURUGENZI Mtendaji wa Muungano wa klabu za waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Kenneth Simbaya (wa pili kushoto) akieleza jambo kwa Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoa Kigoma (KGPC) ambaye pia ni Rais wa UTPC, Deogratias Nsokolo (kushoto) na Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Jacob Ruvilo alipowasilili klabuni hapo kwa ziara maalum hivi karibuni.

“Zipo taarifa za waandishi wengi kufanyiwa madhila na wadau yakiwemo ya kushushwa njiani katika ziara, vitisho, ubaguzi na unyanyapaa mambo ambayo yanakwamisha ufanisi wa Mwandishi kuripoti habari kwa maslahi ya umma”, alieleza Simbaya.

Alieleza kuwa UTPC kwa kushirikiana na wadau wengine wa habari inazingatia ulinzi na usalama wa waandishi wa habari wanapokua kazini hivyo ni vyema nao wakashiriki kwa kutoa taarifa pindi wanapofikwa na madhila iwe ndani ya vyombo vyao au wadau wengine.

MAKAMU Mwenyekiti wa KGPC, Jacob Ruvilo, akitoa maelezo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Kenneth Simbaya, alipotembelea ofisi za klabu hiyo hiyo hivi.

Akizungumzia mkakati wa UTPC, Simbaya alieleza kuwa unalenga kuleta mabadiliko chanya na ufanisi kwa klabu zote hivyo waandishi wa habari wanapaswa kuziunga mkono klabu kwa kujiunga nazo na kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya kazi zao.

Akizungumzia ziara hiyo, Katibu wa KGPC, Mwajabu Hoza, alieleza wananchama na waandishi wa mkoa huo wamefarajika kutembelewa na kiongozi huyo ambaye alitoa elimu na taarifa zinazoonesha matumaini ya kuimarika kwa klabu na tasnia ya uandishi wa Habari nchini.

MKURUGENZI Mtendaji wa Muungano wa klabu za waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Kenneth Simbaya akizungumza na waandishi wa habari, wanachaka wa KGPC alipofika katika ofisi za klabu hiyo hivi karibuni.

Aidha alimpongeza kiongozi huyo na ujumbe wake pamoja na wanachama wa klabu hiyo akiwemo Mwenyekiti ambaye pia ni Rais wa UTPC, Deogratias Nsokolo, kwa kujitokeza na kuhudhuria shughuli mbali mbali katika ziara hiyo.

Simbaya aliyeajiriwa mwezi Agosti mwaka jana katika nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji, mbali ya kusimamia mageuzi na kazi za UTPC akiwa makao maku Dodoma, amekua akifanya ziara za kutembelea klabu za waandishi wa habari Tanzania bara na Zanzibar kueleza mipango na mikakati ya kuinarisha klabu na tasnia ya uandishi wa habari nchini.

 

Comments

Popular posts from this blog

Balozi Mpanda ahimiza ubunifu uhifadhi wa mazingira

Vodacom yawapa uhakika wa matibabu mama, watoto wachanga