Wahariri chachu ya maendeleo, ukuaji wa Kiswahili - Hemed
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, ameeleza kuwa juhudi za wahariri wa vyombo mbali mbali vya habari zimechangia ukuaji na maendeleo ya lugha ya Kiswahili ulimwenguni.
Hemed ameyasema
hayo katika mkutano wa wahariri wa vyombo vya habari wa Tanzania kuadhimisha Siku
ya Kiswahili Duniani uliofanyika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni jijini
Zanzibar.
Amesema Wahariri Wakuu wana jukumu la kupitisha na kuweka sawa maandishi yote ndani ya vitabu, magazeti, majarida na vipindi vya redio au televisheni hatua iliyosaidia kwa kiasi kikubwa kukuza lugha hiyo ndani na nje ya Tanzania.
Aidha amewataka kuendelea kuzingatia maadili ya
kazi zao na kuibua mambo yasiyoendana na mila, tamaduni na silka za nchi bila
ya kumuonea mtu au taasisi muhali.
Hemed pia alitumia
jukwaa hilo kueleza fursa zinazopatikana katika lugha ya Kiswahili na kuwataka
wenye ujuzi wa lugha hiyo kuzichangamkia ikiwemo ukalimani, utafsiri, uhariri,
uandishi na utangazaji wa habari pamoja na ufundishaji wa lugha hiyo kwa
wageni.
Aidha ameeleza kufurahishwa kwake na juhudi zinazochukuliwa na Baraza la Kiswahili la Tanzania (BAKITA) na Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) ya kuieneza lugha hiyo katika mataifa mbali mbali ulimwenguni.
“Juhudi hizo
zinaenda sambamba na mikakati ya kukifikisha Kiswahili katika nchi mbali mbali ikiwemo
ya Ujerumani, Uholanzi, Italia, Nigeria, nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu
(UAE), Malawi, Rwanda na Zimbabwe hatua ambaZo ni dhahiri zinaongeza umahiri wa
watumiaji wa lugha hii katika mataifa yao”, amesema Hemed.
Kwa kuzingatia ukubwa
na kuendelea kutapakaa kwa lugha hiyo, Hemed amelitaia Jukwaa la Wahariri Tanzania
na wahariri wa vyombo mbali mbali vya habari, kuendelea kushirikiana na mabaraza
ya Kiswahili nchini kuhakikisha vyombo vya habari vinatumia kiswahili fasaha na Sanifu.
Pia ameeleza kuwa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi
imeamua kuifanyia marekebisho Sheria ya Habari ili iendane na mabadiliko yanayotokezea
katika sekta ya mawasiliano na teknolojia ya habari nchini.
Kwa upande wake
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo, Tabia Maulid Mwita, ameeleza kuwa serikali zote mbili za Tanzania zina
mkakati wa kukifanya Kiswahili kuwa ni bidhaa itakayowanufaisha wataalamu wa
lugha hiyo na taifa kwa ujumla.
Alitaja baadhi ya
manufaa hayo kuwa ni pamoja na kupeleka
walimu wa kusomesha Kiswahili nje ya Tanzania pamoja na kuwakaribisha wageni
kusoma Lugha hiyo katika vyuo na taasisi za elimu zilizopo nchini.
Aidha Tabia amewataka
Wahariri Wakuu kukemea tabia ya wachache wanaotumia misamiati kinyume na maana
zilizokusudiwa ili kudhibiti ufasaha wa lugha.
Nae Naibu Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Khamis Mwinjuma, ameeleza kuwa Serikali zote mbili za Tanzania zinachukua jitihada katika kuhakikisha lugha ya Kiswahili inakuwa ni nembo ya taifa la Tanzania.
Amesema ni wajibu
wa wananchi kuhakikisha wanaitangaza Lugha ya Kiswahili ikiwemo kuibua Utalii
wa Lugha ya Kiswahili ili kuhakikisha wageni wanaotembelea Tanzania wanatumia
fursa zitokanazo na Lugha hiyo.
Akitoa maelezo
kuhusu jukwaa hilo Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Tanzania (BAKIZA),
Consolata Mushi ameeleza kuwa Jukwaa hilo litakuwa ni chachu ya kupunguza
changamoto za Kiswahili zinazojitokeza katika vyombo vya habari na kuchochea
usanifu wa lugha.
Katika mkutano huo,
pia wahariri na wadau wa lugha ya Kiswahili walipata nafasi ya kuelezea njia na
mbinu mbali mbali za kupunguza makosa yanayofanywa na waandiushi na watangazaji
wa vyombo vya habari.
Mkurugenzi wa Idara
ya Mawasiliano Ikulu Zanzibar ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar, Charles Martin Hilary, alieleza haja ya watangazaji wa redio na
televisheni kuzingatia usanifu na ufasaha wa lugha wanapokuwa kwenye vipindi
kuepusha ubanangaji wa lugha ya Kiswahili.
Aliongeza kuwa wapo
watangazaji wanaochanganya lugha ya Kiswahili na kiingereza jambo linaloondoa
ladha na kupotosha maana na uhalisia wa maneno ya Kiswahili.
Comments
Post a Comment