ZAMECO yakerwa na video ya udhalilishaji mtandaoni
NA MWANDISHI WETU
KAMATI ya Wataalamu wa Masuala ya Habari Zanzibar
(ZAMECO) inayoundwa na taasisi za kihabari na wadau wa habari imelaani video
inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii inayoonesha wasichana wawili
waliorekodiwa na kuulizwa maswali yasiyo na maadili, kuvunja heshima na kukiuka
haki za binaadamu.
Taarifa iliyotolewa na taasisi hizo na kutiwa saini kwa pamoja na mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC), Abdallah Mfaume na Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA ZNZ), Dk. Mzuri Issa, ilieleza kuwa tukio hili limeibua hisia kali kwa wadau wa habari, watetezi wa haki za binaadamu najamii kwa ujumla.
Ilielezwa kuwa
tukio hilo pia limeibua maswali yasiyo na majibu miongoni mwa wanahabari kuhusu
maadili, haki za binadamu, na misingi ya uhuru wa vyombo vya habari.
“Hivyo basi ZAMECO
inasisitiza kuwa vitendo vya udhalilishaji kwa watoto wa kike na jamii ni
ukiukwaji wa haki za binaadamu, maadili ya uandishi wa habari na kuvuruga mipaka
ya uhuru wa kujieleza ambao unalindwa na unahitajika kwa lengo la kutoa habari
sahihi kwa lengo kuibua mijadala yenye tija na manufaa kwa jamii”, ilieleaza
taarifa hiyo.
Ilielezwa kuwa kwa
mujibu wa Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR 1996)
Ibara(19) inayoeleza kuwa ‘kila mtu ana uhuru wa kutoa taarifa bila ya kuathiri
haki ya mtu na amani ya nchi’.
“Hii ina maana
kuwa uhuru wa vyombo vya habari unaendana na jukumu la kuheshimu utu wa kila
mtu, hasa wanawake na vijana ambao ni waathirika wa moja kwa moja katika hatari
yoyote itakayotokea, hivyo ZAMECO inaziomba Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
(TCRA) na Tume ya Utangazaji Zanzibar kuhakikisha maudhui yanayorushwa na
mitandao ya kijamii yanaendana na viwango vya maadili, uwajibikaji na kulinda
jamii dhidi ya maudhui yenye madhara kwao”, ilieleza taarifa hiyo.
Aidha ZAMECO iliiomba
Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo Zanzibar kuharakisha upatikanaji
wa sheria mpya ya huduma za habari nchini kwa lengo la kupunguza changamoto
kama hizo kwani ukizingatia mapendekezo ya sheria hiyo yaliyoelezea kwa kina
nani muandishi wa habari, sifa zake na kazi zake kwa ujumla.
Aidha kamati hiyo
ilisisitiza umuhimu wa wasichana kujitambua, kujithamini na kujiwekea malengo
yatakayoimarisha maisha yao kwani kufanya hivyo kunawapa uwezo wa kufanya
maamuzi sahihi, kujiamini na kuepuka kutumiwa kwa maslahi yanayoweza
kudhoofisha ndoto zao.
ZAMECO pia iliwaomba
wazazi na walezi kuwa mstari wa mbele katika kuwaelimisha watoto wao wa kike
juu ya thamani yao, haki zao na nafasi yao katika jamii sambamba na
kuwaelimisha vijana wa kiume kuwaheshimu watoto wa kike na kuwajengea mazingira
yenye maadili mema.
Kamati hiyo inaundwa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA - Zanzibar), Baraza la Habari (MCT), Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA), Jukwaa la Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC Zanzibar), Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC) na Klabu ya Waandishi wa Habari Pemba (PPC).
Comments
Post a Comment