ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

NA MWANDISHI MAALUM, WKUMM

WIZARA ya Kilimo Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana na wadau mbali mbali kupitia taasisi zake kustawisha sekta ya kilimo na ufugaji.

Waziri wa wizara hiyo, Shamata Shaame Khamis alieleza hayo baada ya kushuhudia utiaji saini ya makubaliano ya ushirikiano na kiutendaji kati ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Zanzibar (ZALIRI) na taasisi ya Friedrich Loeffler Institut (FLI) ya nchini Ujerumani. 

Katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa ZARILI, Talib Saleh Suleiman alitia saini kwa niaba ya taasisi hiyo na kwa upande wa  FLI, Mkurugenzi wa Institute of International Animal/One Health, Prof. Sascha Knauf aliiwakilisha taasisi yake.

Waziri Shamata  alieleza kuwa  serikali ya Ujerumani imekuwa na ushirikiano wa karibu na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi  Zanzibar katika mipango yake ya maendeleo. 

Alifahamisha kuwa utiaji saini huo utaongeza ufanisi na wataalamu wa utafiti wa masuala ya mifugo lakini pia kubadilishana uzoefu  kati ya nchi mbili hizo .

Alisema mashirikiano baina ya taasisi hizo kunatoa mwanga wa kuzipatia ufumbuzi   katika masuala ya tafiti kupitia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazoikabili sekta ya mifugo .

Alisema sekta mifugo imegusa moja kwa moja wananchi hususani katika mambo ya afya kwani hivi sasa wanyama wamekua wakisababisha maradhi kwa binadamu hivyo kufanyika kwa tafiti za mara kwa mara kutaondoa changamoto hizo.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kushirikiana na ya Ujerumani kupitia tasisi hiyo katika mpango wa kubadilishana uzoefu kuhusu mifugo ili kuona sekta hiyo inazidi kuimarika.

Awali Mkurugenzi wa ZARILI, Talib Saleh Suleiman, alisema mkataba huo una lengo la kushirikiana na kusaidia katika masuala ya maendeleo ya mifugo.

Alifahamisha kuwa taasisi hiyo ya Ujerumani itawafundisha watendaji wa ZARILI mbinu za kuimarisha mifugo na ufugaji wa kisasa zaidi kwa manufaa ya watu wa Zanzibar.

Aliongeza kuwa mashrikiano hayo yaisaidia taasisi yake itazidi kupata maendeleo hasa katika masuala ya utafiti,  kuimarisha maabara na kujua mambo mbali mbali yanayohusu mifugo. 

Kwa Upande wake Prof. Knauf alieleza kuwa Serikali ya  Ujerumani inajivunia ushirikiano kati yake na  Zanzibar hivyo taasisi yake itaendelea kutoa kila aina ya usaidizi kufikia azma ya maendeleo ya nchi na watu wake.

Alisema kupitia makubaliano hayo, ana amini ya kwamba yataenda kuimarisha mifugo na utafiti wake na kuleta mbinu bora za ufugaji ili kuleta mafanikio makubwa nchini.

Comments

Popular posts from this blog

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango