ABSA kuendelea kuchangia kampeni uzazi salama Z'bar
NA MWANDISHI WETU
BENKI ya ABSA Tanzania imeeleza kuwa itaendelea
kushirikian na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kustawisha afya za wananchi wa Zanzibar kupitia kampeni na programu mbali mbali.
Akizungumza baada ya matembezi
ya hiyari na mbio fupi za marathoni (Wogging) zilizoandaliwa na shirika la AMREF Tanzania kwa
lengo la kusaidia jamii kupitia sekta ya afya, Mkurugenzi Mtendaji wa benki
hiyo, Obedi Laiser, alisema wameamua kudhamini tukio hilo kwa kutambua juhudi
zinazochukuliwa na serikali kuiimarisha sekta hiyo.
“Sisi kama benki tunatambua
mchango mkubwa mashirika binafsi kama AMREF mnafanya katika kuleta mabadiliko
katika jamii na ndio dhumuni kuu kwetu kutamani kushiriki na kuunga jitihada
hizi za kuleta mabadiliko katika afya ya uzazi wa mama na mtoto”, alieleza
Mkurugenzi huyo.
Aliongeza kuwa dhumuni ya
benki hiyo kushiriki kwenye tukio hilo ni kuchangia na utatuzi wa changamoto na
vikwazo ambavyo wanawake wajawazito mara nyingi hukumbana nazo wakati wa
kujifungua.
Aidha Mkurugenzi huyo alieleza kuwa jitihada ya pamoja kuongeza uelewa na kuelewa kuhusu changamoto na tabu wanazopitia wanawake wajawazito zinahitajika ili pia kutatua dharura zinazowapata watoto pindi wanapozaliwa.
“Lengo la ABSA ni kuiwezesha Afrika ya kesho, pamoja, mtu mmoja
baada ya mwengine. Katika kutafuta jamii yenye afya bora na mustakabali
mzuri, lazima tukubali umuhimu mkubwa wa afya ya mama na mtoto”, alieleza.
Alifafanua kuwa tukio hili
ni jukwaa la wadau wa sekta ya afya kuangazia changamoto zinazowakabili mama
wajawazito ili kuhamasisha mabadiliko chanya kwa kuchochea uelewa na huruma
kubwa ndani ya jamii yetu.
“Wanawake wajawazito ni
msingi wa kizazi chetu cha baadaye. Ustawi wao unaathiri moja kwa moja afya na
uwezo wa kizazi kijacho cha watu ambao wataunda nchi yetu na ulimwengu kwa
ujumla”, alieleza.
Alifafanua kuwa benki hiyo
imedhamini tukio hlo kwa kutoa Shilingi milioni 100 ambazo zitasaidia upatikanaji wa
vifaa tiba vitakavyofanikisha uzazi salama kwa mama na mtoto.
Aidha alipongeza juhudi za Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwa jitihada inazochukua kuleta maendeleo kwa watu wa
Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Akihutubia katika tukio
hilo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi,
aliipongeza benki hiyo kwa kudhamini na kufanikisha matembezi na mbio hizo zenye
lengo la kuimarisha huduma za afya ya uzazi salama wa mama na mtoto.
“Kwa niaba ya serikali
natoa shukurani kwa benki ya ABSA Tanzania na kuwataka waendelee kutupa ushirikiano
katika kuhakikisha tunafanikiwa katika malengo yetu ya kupunguza idadi ya vifo
vya mama wajawazito na watoto vinavyotokana na uzazi”, alieleza Dk, Mwinyi.
Aidha Dk. Mwinyi alieleza kufurahishwa
na kampeni ya miaka mitatu na iliyoanza tokea mwaka jana ikiwa na lengo la
kukusanya shilingi bilioni moja ambapo hadi sasa ahadi za jumla ya shilingi milioni
792 zimetolewa huku shilingi milioni 557.
Alisema, kampeni ya Uzazi
Salama inaunga mkono juhudi za serikali kupunguza na kuepusha vifo vya mama
wajawazito na watoto wachanga kutokana na ukweli kuwa bado takwimu za vifo
hivyo bado vipo juu.
“Takwimu zinaonesha vifo
vya kina mama 134 kati ya vizazi hai 100 kwa mwaka na vifo 28 vya watoto
wachanga kati ya vizazi hai 1,000 kwa mujibu wa takwimu za utafiti wa afya ya
uzazi na mtoto na viashiria vya malaria Tanzania (TDHS) za mwaka 2017”, alisema
Dk. Mwinyi.
Aliongeza kuwa kiwango
hicho kinasababishwa na changamoto mbali mbali zikiwemo za upungufu wa vifaa
tiba, uhaba wa wahudumu pamoja na kukosekana kwa dawa.
Matembezi ya hiyari na mbio
fupi za AMREF Wogging Marathon 2023 zimefanyika kwa mara ya pili Zanzibar zimeandaliwa
na shirika hilo kwa ushirikiano na serikali huku benki ya ABSA ikiwa mdhamini mkuuu
sambamba na taasisi mbalimbali, wananchi pamoja na wadau wengine waliochangia fedha, vifaa na utaalamu
kuzifanikisha.
Comments
Post a Comment