Dimwa azionesha fursa za kilimo jumuiya CCM
NA mWANDISHI WETU
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dk. Mohammed Said Mohammed ‘Dimwa’, amezishajihisha jumuiya za CCM kuyatumia mashamba ya chama hicho kulima kilimo cha kisasa ili kujipatia ajira.
Dk. Dimwa alieleza hayo mara baada ya kutembelea mabanda ya maonyesho ya wakulima nane nane huko katika viwanja vya Dole Kizimbani, wilaya ya Magharibi ‘A’ Unguja.
Alisema CCM ina mashamba makubwa na moja katika malengo yake ni kuwekekeza katika kilimo hivvo ni fursa sasa kwa vijana na jumuiya zote za chama ambao wanataka kujiunga na kilimo kuyatumia sasa mashamba hayo.
“CCM ina mashamba mengi yakiwemo ya Kilombero, Kiwengwa na Bumbwini lakini la kilimo hasa ni hili la Kilombero na tuna heka nyingi waende kwenye maonesho kupata elimu ili waweze kuyatumia na wajiajiri kama inavyoelekezwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ili kuepuka kukaa bila ya kazi maalum,” alisema.
Aidha alisema, chama kimeshazungumza na benki ya kilimo kwa ajili ya
kuwafadhili na imekubali kupitia mashamba yao na CCM kwa ujumla inaweza
kukopesheka.
"Sasa tunawashajihisha sio tu vijana lakini jumuiya zote kama wazazi na
kina mama kwa nafasi yao kwenye mashamba yale kila mtu atakaye taka kulima basi
anaruhusiwa na tutaanza hapo katika ajira zetu za chama," alisema.
Akizungumzia maonesho ya wakulima, alisema yanatoa fursa kwa wananchi kupata uelewa
juu ya kilimo cha kisasa.
Alisema maonesho hayo yanatoa nafasi kwa Wazanzibari kupata uelewa juu ya kilimo na kutoka katika kilimo cha mkono na kwenda katika kilimo cha kisasa ili kiweze kuwaletea tija.
Hata hivyo, alisema kupitia kilimo
cha kisasa basi wakulima watapata mazao mengi na yaliyobora kwa kutumia sehemu
ndogo ya shamba au bustani.
"Zanzibar ardhi haikui lakini watu wanaongezeka hivyo kwa kupitia kilimo
cha kisasa tutapata kulima mazao yetu katika eneo dogo na kupata mazao
yaliyomengi," alisema.
Alibainisha kuwa hivi sasa mambo
mengi yanarahisishwa kwani unaweza kupima udongo ili kujua kama udongo huo
unafaa kwa kutoa mazao bora.
Sambamba na hayo, alisema maonesho hayo yanaleta hamasa katika sekta na mifugo
kwa kuwavutia wananchi wengi kuingia katika sekta hizo kwani kupitia maoenysho
hayo wananchi wanapata kuona juu ya kilimo cha kisasa ambacho hakitumii nguvu
nyingi.
Hivyo, aliiomba Wizara ya Kilimo,
Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo kuendelea kuratibu vizuri jambo hilo na
kuwashajihisha wananchi kutembelea kwa wingi maonyesho hayo ili waweze kupata
elimu ambayo itawasaidia kuingia katika kilimo chenye tija.
Comments
Post a Comment