TADB yawaonesha fursa wakulima, wavuvi

NA MWANDISHI WETU

MKURUGENZI Idara ya Kilimo na Uhakika wa Chakula, Hamad Masoud Ali (wa kwanza kulia), amesema kuna umuhimu mkubwa kwa wakulima hapa nchini kutumia fursa mbali mbali zikiwemo za mikopo ili kuongeza uzalishaji wa mazao.

Mkurugenzi huyo alieleza hayo, kwenye hafla ya ufunguzi wa semina iliyowashirikisha wakulima, wafugaji na wavuvi, hafla iliyofanyika katika viwanja vya maonesho ya kilimo vilivyopo Dole.

Alisema ili wakulima, wafugaji na wavuvi wapige hatua, lazima wawe na uhakika wa mtaji, ambapo suala hilo hivi sasa limerahisishwa kwani upo uwezekano wa kuchukua mikopo kwenye taasisi za kifedha.

Alieleza kuwa wakulima wengi wa Zanzibar wamejikita kwenye kilimo cha kujikimu kutokana na kutokuwa na mtaji, hivyo uwepo wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo, utawasaidia kuondokana na changamoto wa mitaji.

Alifahamisha kuwa suala jengine muhimu litakalowafanya wakulima, wafugaji na wavuvi wapige hatua na kupata tija zaidi ni kuhakikisha wanakuwa na elimu ya kutosha kwa sekta wanayoifanyiakazi.

“Tunapozungumia kupata tija kwenye kilimo, ufugaji na uvuvi, kwanza lazima muwe na mitaji ya kuendeleza shughuli zenu, lakini muhimu zaidi ni elimu ya kazi unayoifanya”, alisema Mkurugenzi huyo.

Akizungumzia kuhusu lengo la semina hiyo, mkurugenzi huyo alisema itawasaidia kutambua fursa mbali mbali zinazopatikana kwenye benki ya Maendeleo ya Kilimo, sambamba na kuongeza elimu.

Nae ofisa maendeleo ya Biashara Mkuu Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kanda ya Zanzibar, Ashura Akim (kushoto), amesema taasisi hiyo imeanzishwa kwa lengo la kuwapatia wakulima, wavuvi na wafugaji mikopo itakayowatoa katika kilimo cha kujikimu kwenda kwenye kilimo cha biashara.

Nao washiriki wa semina hiyo wameiomba benki hiyo kuweka masharti nafuu ya mkopo kwani huko nyuma wakulima wengi walishindwa kupata mkopo kutokana na kutokukidhi masharti.

Walisema kuwa miongoni mwa faida za kuwepo maonesho ni pamoja na wananchi kupata elimu kuhusiana na mambo mbalimbali, hivyo waliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupata fursa kama hizo.

Benki ya maendeleo ya kilimo Tanzania (TADB) ni taasissi inayomilikiwa na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ilianzishwa mwaka 2015 ikiwa kwa lengo la kuwapatia mikopo wakulima, wavuvi, wafugaji na watu wote wanaojihusisha na kuongeza thamani mazao yanayotokana na kilimo, ufugaji na Uvuvi.

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango