Dk. Samia awaonya wanasiasa katiba mpya

Asema si mali ya wanasiasa, awataka kutolazimisha upatikanaji wake

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

RAIS wa Jamahuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema katiba si mali ya vyama vya siasa, bali ni ya watanzania wote, hivyo marekebisho yanayohitaji kufanyika lazima kufanyike tafakari kubwa.

Dk. Samia alieleza hayo jana katika ukumbi wa kituo cha mikutano cha Julius Nyerere, Dar es Salaam wakati akifungua mkutano maalum wa siku tatu wa baraza la vyama vya siasa na wadau wa demokrasia. 

Alitumia fursa hiyo kuwataka viongozi wa vyama vya siasa nchini kuacha jukumu la kujimilikisha katiba, kwani si mali yao na kutumia fursa hiyo kuvitaka vyama vikatoe maoni ya katiba.

Alisema maoni yaliyopo kila upande, wamependekeza marekebisho ya katiba kwa upande wa bara na Zanzibar, lakini mchakato wa marekebisho ya katiba si mali ya vyama vya siasa na hivyo wanasiasa waache kuwaburuza wananchi.

“Mchakato wa katiba si mali ya vyama vya siasa, katiba ni ya watanzania, awe ana chama au hana. Katiba ni mali ya watanzania kwa hiyo marekebisho yake yanahitaji tafakuri kubwa sana”, alisema Dk. Samia.

Alisema inawezekana kukufanywa marekebisho ya katiba lakini kwa kiasi gani wananchi wanafahamu yaliyoandikwa kwenye kitabu cha katiba na kushauri kwanza umuhimu wa elimu ya katiba.

“Katiba ni kitabu, tunaweza tukatengeneza katiba kitabu kizuri tukakipamba tukakiweka, lakini wangapi wanaelewa yaliyomo ndani ya kitabu, kitabu tulichonacho sasa wangapi wanakielewa? unakwendaje kumuuliza mtanzania nipe maoni yako kitu hakijui tunaanza na elimu”, alisema.

Aidha Dk. Samia alisema kuna uhuru wa maoni, hata hivyo hakuna uhuru usio na mipaka sio kisheria pekee bali hata kibinadamu, lakini inahitaji uungwana kufahamu mipaka hiyo.

Akizungumzia kuhusu ruhusa ya kufanya mikutano kwa vyama vya siasa alisema lengo lilikuwa kuvipa nafasi vyama hivyo vikanadi sera kwa wananchi ili ukifika uchaguzi vyama viwe vimesimama vizuri.

Hata hivyo alisema jambo la kushangaza ni kwamba vyama hivyo vimeacha kueleza sera kwa wananchi badala yake wanakwenda kuvunja sheria, kutukuna, kukashifu na kuchambua dini za watu.

“Lakini sishangai kwanini haya yanatokea, kwa sababu ya kuzungumzwa hakuna. Tulianza katiba ikakatika katikati, ikaja bandari, sasa katiba tena. Hakuna cha kuzungumzwa na unalazimisha lazima ufanye jambo”, alisema Samia.

Alisema uendeshaji wa Tanzania unahitaji fikra za kila mtu na kwamba hakuna mtu mwenye waraka ama hati ya umiliki wa Tanzania na kwamba nchi ni ya watu wote, hivyo tofauti zilizopo zisiwe kigezo cha kuipeleka nchi kusiko na faida.

Alidokeza kuwa hakuna fomula ya demokrasia inayofafana ulimwenguni na hata nchi za Afrika jumuiya ya Afrika Mashariki kila taifa lina mila, desturi na tamaduni zake, zinazohitaji kufuatwa kama ilivyo Tanzania katika kulinda maadili yetu.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama alisema ajenda ya demokrasia ya vyama vya siasa ni kuhakikisha amani na utulivu unalindwa.

Naye Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi alisema watajadili hali ya siasa nchini na mapendekezo yatayotokewa yatafanyiwa kazi, pamoja na kumshukuru Rais Samia kudhamini mkutano huo kufanyika.



 

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango