KCFZ yasaidia kambi za wanafunzi Fujoni

NA MWANDISHI WETU

TAASISI na mashirika ya ndani na nje ya nchi zimetakiwa kutoa misaada kwa wanafunzi wanaojiandaa na mitihani ya taifa ili kurahisisha juhudi za walimu za kuhakikisha wanafunzi wanapata matokeo mazuri.


MENEJA wa taasisi ya Korea Culture Foundation for  Zanzibar (KCFZ), Jenipher Barnaba Marcus akizungumza na wanafunzi waliopo katika kambi ya masomo skuli ya Fujoni wakati walipofika kutoa msaada wa chakula na vyandarua kwa wanafunzi wa skuli hiyo.

Wito huo umetolewa na Mwalimu Mkuu skuli ya Fujoni, wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja, Abdu Maulid Fidia, alisema hayo skulini hapo mara baada ya kupokea msaada wa mchele na vyandarua vilivyotolewa na taasisi ya utamaduni ya Korea (Korea Calture of Zanzibar - KCFZ).

Alisema wanafunzi wanaojiandaa na mitihani kwa kukaa kambi wana mahitaji mengi yakiwemo ya vyakula hivyo kujitokeza kwa wadau hao kutasaidia upatikanaji wa mahitaji kwa wanafunzi.

Aidha alisema baadhi ya wanafunzi wameshindwa kukaa kambi kutokana na kutomudu gharama za huduma zikiwemo za chakula.

Mwalimu huyo alisema wanafunzi 120 wa skuli hiyo wameshindwa kukaa kambini kati ya wanafunzi 198 wanaojiandaa na mitihani ya kidatu cha pili na cha nne.

“Tunawaomba wahisani wajitokeze kuwasaidia wanafunzi wetu kwani wanafunzi wengi wanaojiandaa na mitihani wameshindwa kutokana na hali ngumu za maisha”, alisema mwalimu Abdu.

Alifafanua kuwa kila mwanafunzi aliyepo kambini anatakiwa alipe shilingi 250,000 kwa mahitaji ya chakula na mahitaji mengine hivyo kujitokeza kwa wafadhili watasaidia kupunguza kilio hicho kwa wanafunzi.

Sambamba na hayo aliwataka wanafunzi kutumia muda wao vizuri kujiandaa na mitihani sambamba na kuongeza bidii katika kipindi hichi ili kuweza kufanya mitihani yao vizuri hapo baadae.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa taasisi ya KCFZ, Dk. Master Kim, alisema msaada huo utawasaidia wanafunzi kupata chakula pamoja na kutumia vyandarua kujikinga na mbu wanaosababisha malaria.

Hata hivyo aliwataka wanafunzi hao kutumia msaada huo kama ilivyokusudiwa ili kupata mahitaji yao huku Meneja wa taasisi hiyo, Jenipha Barnaba, alisema lengo la kutoa msaada huo kuwasaidia wanafunzi kumudu gharama wakati watapapokuwa kambini na kusema wataendelea kusaidia huduma nyengine hadi wanafunzi hao watakapomaliza mitihani.

Baadhi ya wanafunzi wa skuli hiyo waliishukuru taasisi hiyo kwa kujitokeza kutoa msaada huo na kuzitaka taasisi nyengine kuiga mfano wa taasisi hiyo ya kutoa misaada kwa wanafunzi.


 

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango