Tutaendelea kuzipatia ufumbuzi changamoto za wananchi – Ayoub

NA MADINA ISSA

MKUU wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud, amesema ataendelea kushirikiana na watendaji wanaosimamia sekta mbali mbali ili wananchi wa mkoa huo waendele kupata maendeleo.


MKUU wa mkoa wa Kaskazini Unguja,Ayoub Mohammed Mahmoud (wa pili kushoto) akimsikiliza sheha wa shehia ya Mangapwani wakati wa kikao cha kusikiliza changamoto za wananchi wa mkoa huo.

Akizungumza na wananchi katika kikao cha kusikiliza changamoto kwa wananchi wa kijiji cha Bumbwini, wilaya ya Kaskazini ‘B, alisema baadhi ya changamoto zimekuwa zikipatiwa ufumbuzi ili wananchi wafaidike na huduma.

Alisema serikali ya awamu ya nane imekuwa na lengo la kufikisha huduma muhimu kwa wananchi wake, hivyo aliwahakikishia wananchi kuendelea kushirikiana nao ili kuona huduma hizo zinawafikia kwa wakati.

Akizungumzia suala la wananchi kuendelea kunufaika na rasilimali zilizopo ndani ya mkoa huo, aliwataka wananchi wa Shehia hiyo kusubiri kwa muda wa wiki mbili kutatua changamoto zilizopelekea kufungwa kwa shughuli za uchimbaji wa mawe katika eneo lao.



"Tatizo hili tumeshakaa na tumeshalizungumza lengo letu sio kuwatesa wananchi lengo letu ni kuona mnaendelea kufanya shughuli zenu na kukidhi maisha yenu na familia zenu", alisema.

Aliwataka wananchi wakati litakapofunguliwa shimo hilo, kufuata taratibu zitakazowekwa ikuepuka kufungiwa tena na kusema kuwa viongozi wa taasisi husika watafika ili kuonesha maeneo yatakayoweza kuchimba mawe kwa sehemu ya Bumbwini.

Akizungumza suala la daraja aliwahakikishia kujengwa daraja hilo ili kunusuru maisha ya watu na kuahidi kufuatilia wananchi waliotoa sehemu zao kwa ajili ya uchimbaji wa kifusi kulipwa fidia zao.

Kuhusu huduma za afya, Ayoub alisema serikali inaendelea kuimarisha huduma hizo kwa kuimarisha majengo ya kuolea huduma, upatikanaji wa vifaa na vipimo na pamoja na dawa kwa uhakika kwa lengo la kuwafikishia huduma za uhakika.

Mapema, baadhi ya wananchi washehia hiyo, walisema wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo ya kuzuiwa kuchimba mawe jambo linalowapelekea wananchi na vijana kuingia katika vikundi viovu.

 Pia wananchi hao walisema kuwa pia kuna changamoto ya kutolipwa fidia kwa baadhi ya wananchi waliotoa sehemu zao kwa ajili ya kupisha ujenzi, na kumtaka mkuu wa mkoa kuingia kati suala lao hilo ili kuweza kupata haki zao.

"Hatukatai maendeleo na ndio tumepisha maeneo pale tumapotakiwa kufanya hivyo ila kinachotusikitisha sisi wengine hatujalipwa fidia zetu na ni madai ya siku nyingi", alisema Masoud Haji Ussi.

Ussi alidai kuwa hajalipwa fidia kutokana na ya ujenzi wa barabara ya Bumbwini Kiongwe alieleza kuwa hatua hiyo inawavunja moyo licha ya kuthamini juhudi zinazochukuliwa na serikali hivyo alimuomba mkuu huyo wa mkoa kumsaidia kupata fidia hiyo.

Mkuu huyo akiambata na maofisa wa taasisi wa ngazi mbali mbali yupo katika ziara iliyopewa jina la ‘Shehia Tour’ inayolenga kuwakutanisha moja kwa moja wananchi na viongozi wa mkoa kusikiliza na kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo yao.

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango