Utafiti kuimarisha zao la mwani unahitajika - Mama Mariam

NA MWANDISHI WETU

MWENYEKITI wa Bodi ya Wadhamini wa taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), Mama Mariam Mwinyi, ametoa rai ya kufanyiwa utafiti wa zao la mwani ili kulitambulisha zaidi duniani.

MKE wa Rais wa Zanzibar mama Mariam Mwinyi (kulia), akimsikiliza rais wa Jumuiya ya Mapinduzi ya Kijani Barani Afrika (AGRA), Dk. Agnes Kalibata, mazungumzo hayo yaliyofanyika jana katika ukumbi mdogo wa jengo la mikutano la kimataifa la Julius Nyerere jijini Dar es salaam.

Mama Mariam alitoa rai hiyo alipozungumza kwenye mkutano wa kimataifa unaojadili mfumo wa chakula kwenye mada ya nafasi ya mwanamke kwenye sekta ya kilimo na chakula, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa kimataifa la Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Alisema Zanzibar ni nchi inayoongoza barani Afrika kwenye uzalishaji mwani na inakamata asilimia tatu ya pato la taifa baada ya utalii unaochangia asilimia 30 ya pato la taifa na kilimo cha karafuu.

Alisema, asilimia 70 ya dunia ni bahari na 30 ni ardhi hiyo alisema Zanzibar ina eneo kubwa la kulima mwani bado halijatuka, hivyo aliitaka jamii kujikita zaidi kwenye kilimo hicho kwani kinafursa nyingi za uchumi na maendeleo.

Mama Mariam Mwinyi alieleza taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation inaunga mkono jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia sera yake ya Uchumi wa Buluu unaoshajihisha wananchi zaidi kuzitumia fursa ya bahari kwa kuleta maendeleo ya kiuchumi na kujiongezea kipato.

Alisema ZMBF imewawezesha kiuchumi wanawake na kinamama wakulima wa mwani baada ya kuwaweka pamoja vikundi 16 vya kinamama 20 kwa Unguja na Pemba kwa lengo kuwapa mikopo nafuu ili kuendeleza zao hilo.

“Kilimo cha mwani Zanzibar asilimia 90 ya wakulima wake ni wanawake, ZMBF imewawezesha ili kiwaletee tija baada ya kujikita kwenye kilimo hicho kwa zaidi ya miaka 15 nyuma bila ya mafanikio kwa kuwapa vifaa (Chanja za kuanikia Mwani), mafunzo na mbinu za kisasa za ukulima huo”, alifafanua Mama Mariam Mwinyi.

Akitaja faida ya zao la mwani mama Mariam Mwinyi alieleza mwani unaongoza kuwa na virutubisho vingi kuliko mazao mengine, hutumiwa kwa mapambo na kutengenezewa urembo huko duniani pia husaidia lishe kwa watoto na mama wajawazito kwani jamii ikitumia zao hilo kama chakula linasaidia kwa madini ya chuma ambayo ni muhimu kwa afya ya binaadamu.

Alisema, Zanzibar ina changamoto ya utapiamlo kwa watoto wadogo hivyo aliiomba jamii kuweka utamaduni wakutumia bidhaa zilizosarifiwa kwa zao la mwani ili kujiepusha na tatizo hilo na kueleza kati ya watoto watano wanaozaliwa mtoto mmoja hukumbwa na tatizo la utapiamlo na kuwataka kina mama wajawazito kutumia kwa wingi bidhaa zinazotokana na zao la mwani.

Alisema, mbali ya changamoto nyingi wanazokumbana nazo wakulima wa zao hilo, ikiwemo kulima mwani usiokuwa na ubora, kutokuwa na mashine za kusarifia mwani wenye kiwango kwa ajili ya kuuza kwa bei ya juu zaidi.

Waziri wa Maendeleo anayeshughulikia masuala ya kimataifa nchini Norway, Anne Beathe Trinnereim, alieleza kwenye mkutano huo namna wanavyowasaidia wajasiarimali wadogo nchini humo kuwainua kiuchumi na kuwawezesha wanawake kutimiza ndoto zao za maendeleo.

Alieleza jinsi serikali ya Norway ilivyoweka mikakati ya kukabiliana na njaa na utapiamlo kwa kuwashajihisha wananwake wa vijijini kuongeza jitihada kwenye kupeleka mapinduzi ya kilimo na kuimarisha usalama wa chakula kwa kuzitumia vyema fursa za kilimo nchini humo.

Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), iliasisiwa rasmi Febuari mwaka jana, mwezi Machi mwaka huu, ilizindua Mpango Mkakati wa miaka mitatu unaoielekeza kustawisha maisha ya wananchi wa zanzibar hasa vijana na wanawake.  

Aidha, taasisi hiyo inafanya kazi kwa karibu na taasisi za serikali zikiwemo Mahakama ya Zanzibar, Wizara ya Afya, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Wizara ya Uchumi wa Buluu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee Wazee na watoto, Wizara ya Habari na Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda.


Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango