Enezeni elimu kupunguza uharibifu wa misitu – Shamata
NA SALAMA MOHAMMED, WKUMM
WAZIRI wa Kilimo Umwagiliaji Maliasili na Mifugo, Shamata Shaame Khamis, ameitaka Idara ya Misitu kuandaa mafunzo maalum kwa wanajamii, Taasisi za Serikali na Zisizo za kiserikali (NGO's) ili kupunguza uharibifu wa misitu.
Ameeleza
hayo shehia ya Bwejuu katika eneo la hifadhi ya Msitu wa Jamii Tongole, wilaya ya
Kusini Unguja wakati alipokua akizindua zoezi la Upandaji wa miti asili kwenye
msitu huo.
Shamata amesema kuna baadhi ya watu wana mwamko mdogo wa kutunza misitu asili na hivyo kusababisha matatizo yakiwemo ya mabadiliko ya tabia nchi hivyo wakipatiwa elimu itawasaidia kuondokana na uharibifu huo.
Sambamba na hayo alifahamisha kuwa Serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Dk. Hussein Ali Mwinyi ina lengo la kuwasaidia wananchi wake kwa kuwaletea maendeleo hivyo ni wajibu wao kulinda rasilimali zinazopatikana nchini kwa faida ya sasa na baadae.
Hata hivyo alisema licha ya Jumuiya ya Uhifadhi wa Mazingira (JECA) na Idara ya Misitu kuchukua hatua mbali mbali badokuna uharibifu unatokea na kuwaomba watu waliovamia eneo hilo kuondoka na kujisalimisha kabla idara haijachukua hatua.
Nae Mkurugenzi Idara ya Misitu, Said Juma Ali, alifahamisha kuwa upandaji wa miti hiyo unakusudia kurudisha haiba ya eneo hilo ili wananchi waliopo katika eneo hilo kupata kipato na kuwashajihisha kuzingatia sheria kwani atakaekamatwa anafyeka msitu hatua kali za sheria zitachukuliwa.
Kwa Upande wake Naibu Katibu wa Jumuiya Hifadhi ya Mazingira (JECA), Awesu Shaaban Ramadhan, alifafanua kuwa utalii wa misitu ya asili una faida kwa vile rasilimali nyingi zilizomo kama vile ndege na wanyama wengine wanapatikana katika misitu hiyo.
Aliongeza kuwa pindipo wananchi wakiwekeza katika ulinzi na uhifadhi wa misitu hiyo, wataweza kujiingizia wao na serikali mapato hivyo kuondokana na umaskini.
Katika
zoezi hilo, miti 1,300 ya mikunguuni ilipandwa
kwa mashirikiano ya Idara ya Misitu, JECA na jamii katika eneo
hilo, ambapo awali miti 2,300 ilikusudiwa kupandwa lakini kutokana na baadhi
yao kutokukidhi vigezo ya kuwepo katika maeneo ya hifadhi, haikupandwa.
Comments
Post a Comment