Msaada wa kisheria unahitajika kuwaokoa watoto wanaokinzana na sheria

NA AMINA MCHEZO

MSAADA wa watoto kisheria, kisera na kimipango ni uwanja mpana huku ikionekana sheria iliopo Sasa ya mtoto sheria namba 6 ya mwaka 2011 inamapungufu hivyo wizara ya Màendeleo ya jamií, jinsia, wazee na watoto Zanzibar inafanya juhudi kuhakikisha sheria hiyo inapitiwa upya.


Sheria hiyo Kwa Sasa inaonekana bado haitoi ulinzi Bora Kwa mtoto hivyo Kwa Sasa wadau na taasisi za usimamizi wa mtoto wamekuwa wakiisindikiza tume ya marekebisho ya sheria ili kuwe na sheria mpya.

"Kwa Sasa tumeshatoka kwenye hatua nyingi za ukusanyaji wa maoni ya wadau na Sasa nadhani tupo katika hatua ya kuishirikisha tume ya marekebisho ya sheria ili tuone kwamba tunapata baraka za mwisho na kunipeleka mbele ili tuwe na sheria mpya ili mambo yawe mazur Kwa watoto" Amesema mkuu wa wa Division  ya hifadhi ya mtoto kupitia idara ya ustawi wa jamii na wazee.

WASAIDIZI wa Sheria (Paralegal) wakiwa katika moja ya mikutano ya kujengewa uwezo ili watoe huduma bora wa wateja wao.

Mtoto anaekinzana na sheria ni mtoto yeyote alie chini ya umri wa miaka 18 ambae amefanya makosa ya kijinai ikiwemo kubaka, kulawiti, wizi na makosa mengine.

Utafiti umebaini kuwa watoto wengi wanaokinzana na Sheria ni wale watoto wa mzazi mmoja, ndoa kuvunjika, Kukosa matunzo Kwa wazazi wake, hivyo watoto hao hupelekea kuathirika kiakili Kwa kujiingiza katika  makundi maovu na kufanya makosa ya kijinai.

Kiuhalisia kutokana na sababu hizo inaonekana wazi watoto wanaokinzana na sheria wengi wao ni wale waliopitia udhalilishaji Kwa namna Moja au nyengine kutokana na Kukosa malezi sahihi na Kukosa haki zake za msingi kama mtoto.

Msaada wa kisheria Kwa watoto wanaokinzana na sheria umeibua hisia tofauti Kwa wanajamii hasa pale wanapoona makosa ya namna hiyo yakijirudia Kila mara.

MMOJA ya watoa maada wa kisheria akikabidhiwa cheti baada ya mafunzo yaliyotolewa na Idara ya Msaada wa Kisheria Zanzibar. 

Wengine wanasema kupatiwa msaada wa kisheria ni sawa tu kwani wale ni watoto mengi wanayafanya Kwa kutokujua.

Huku mitazamo ya wengine yakionekana kubeba hisia Kali na kukataa kabisa watoto wale kupewa msaada wakidai kuwa ni njia Moja ya watoto hao kuendelea kutenda makosa Kila siku.

"Sioni sababu ya watoto wanaotenda makosa kupewa msaada wa kisheria  kwani nao wanajielewa na wakisaidiwa  kisheria yaani watoto watakuwa wanajiamini Sana", wamesema baadhi yao.

Mtumwa Ameir Ali Msaidizi wa Sheria (Paralegal) kutoka wilaya ya Mjini amesema bado baadhi ya  wanajamii hawajaelewa kuhusu kutolewa Kwa msaada wa kisheria Kwa watoto wanaokinzana na sheria.

Amesema ushawishi wao ni mkubwa Kwa kutafuta wakili wa usimamizi wa kesi za watoto pamoja na wao kumpa elimu na ushauri ili asirudie tena kosa lile.

Amefahamisha kuwa kumuacha mtoto aliekinzana na sheria ni kumkosesha haki zake za msingi ikiwemo kusoma pindi tu atakapokaa chuo Cha mafunzo Kwa Kukosa usaidizi wa kisheria.

"Baadhi ya wajamii hawana uwelewa Kwa sababu wanaona yule mtoto ameshatenda Lile kosa kwanini sisi tunakaa tunamtetea lakini jamii hawajui kuwa Lile kosa linaweza kuwa lisiwe lake au amefanya kosa Kwa ule utoto tu." amesema.

Mtumwa amesema japokuwa sheria haiwaruhusu kusimamia mashauri mahakamani lakini hawawezi kumuacha mtoto aliekinzana na sheria hivyo wanaanza ngazi za awali ikiwemo polisi ili apate haki yake Kwa wepesi na haraka.

Kwa mujibu wa kitengo cha takwimu Dawati la Jinsia Makao Makuu ya polisi Zanzibar kuna kesi 129 zilizoripotiwa na kufikishwa katika mahakama tofauti Zanzibar katika kipindi cha kuanzia Januari Hadi November 2023 zinazowahusu watoto waliokinzana na sheria .

Ripoti hizo zinaonesha kwamba, kesi 70 ni za mkoa wa Mjini Magharibi, 8 mkoa wa Kusini Unguja, 21 mkoa wa Kaskazini Unguja, 16 mkoa wa kusini Pemba na kesi 14 ziliroipotiwa mkoa wa Kaskazini Pemba.

Akizungumza na mwandishi wa makala hii, Mratibu wa Dawati la  jinsia Makao Makuu ya Polisi Zanzibar, Sajenti Rahma Ali Salum, amesema watoto wanaokinzana na sheria wanawaangalia kama watoto wengine hasa katika kuwasaidia kwa kuwapatia elimu ya kujitambua.

Amesema  katika usaidizi wao wa kisheria kwa watoto wa namna hii wanashirikiana na wasaidizi wa sheria, waratibu wa shehia pamoja na ustawi wa jamii  Kwa kusikiliza kesi zao Kwa  pamoja.

Sajenti Rahma amefahamisha kuwa ni wajibu wa watoto wanaokinzana na sheria kupatiwa msaada kutokana na mazingira yanayojitokeza wakati wanapofanya makosa.

"Tukifuatilia kesi zao nyingi ni ushawishi wa watoto wezao, wengine kuwa na njaa kutokana na Kukosa chakula nyumbani ilimradi makosa yao mengi ni ya ushawishitu", amesema Sajenti Rahma.

Ameongeza kuwa Dawati la jinsia wanapopokea kesi za watoto waliotenda makosa wanawaita wazazi wao kuwafahamisha namna ya kukaa na mtoto wake kwani wazazi wengi huwachukia watoto wao kutokana na makosa yao.

"Msaada wa kisheria sana wanapewa na Wasaidizi wa Sheria wanaokuwa pamoja na wazazi wao, sisi tunawafahamisha namna yale makosa yalivyo na mtoto akaenae vipi kwa sababu wazazi wengine wanakua wakali na kuwachukia", amesema.

Amefahamisha kuwa katika kuwasaidia watoto wamekuwa wakipelekwa katika mahakama ya watoto ili wapate uhuru wa kujieleza mbele ya mahakama.

Jumuiya ya wanasheria wanawake Zanzibar ZAFELA ni jumuiya isiyo ya kiserikali ambayo inatoa msaada wa kisheria Kwa wanawake na watoto imesema Kuanzia January Hadi November 2023 jumla ya kesi 11 za watoto wanaokinzana na sheria  zimefika ofisini kwao na wameanza  kuzishughulikia Kwa kuwapatia msaada wa kisheria na kesi 3 tayar zimeshapatiwa ufumbuzi Kwa kutozwa faini.

Mwanaisha Mustapha ni Mwanasheria kutoka Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA)amesema kwa watoto wanaokinzana na sheria wamekuwa wakiwasimamia kwa hali ya juu kwani wengi wao makosa yao ni ya kusingiziwa au ya kulipiziwa visasi Kwa baadhi ya wanajamii waliomzunguka.

Amesema wao kama wanasheria wanasimama kwenye sheria ya mtoto inavyozungumza katika kumlinda kama mtoto mwengine mpaka pale mahakama itakapomtia hatiani Kwa kosa Lile.

Amefahamisha kuwa hali ya sasa asilimia kubwa watoto kwa watoto wanafanyiana udhalilishaji jambo ambalo wanataasisi zinazotoa msaada wa kisheria wamekuwa macho ili  jamii ibaki kuwa salama.

"Ni janga kubwa hali ya udhalilishaji na hali ya sasa hivi iliokuwepo asilimia kubwa watoto Kwa watoto ndio wengi ambao wanafanya haya matukio Kwa iyo tukiwaangali kisheria wote ni watoto na wote wanataka kulindwa na sheria", amesema Mwanaisha.

Aidha Wakili Jamila Massoud kutoka Shirika la Msaada wa Kisheria nà Haki za Binaadam  Zanzibar (ZALHO) amesema wanashuhulikia kesi 19 huku 7 kati yao zikiwa zimeshafikishwa mahakamani Vuga zinazowahusu watoto wanaokinzana na sheria.

Amesema shirika limekuwa na utaratibu wa kuandaa mikutano na wanajamii ili kuzungumza nao na kuwafahamisha kwanini watoto waliokinzana na sheria wanatakiwa kupatiwa msaada wa kisheria.

Amebainisha kuwa pale wanaposhughulikia kesi za watoto wanaokinzana na sheria wanashauri Sana kubadilishiwa makaazi pale anapokuwa tayar ameshakuwa mtoto mwema kwenye jamii ili asirudia tena makosa yale.

"Tunawapa muelekeo au tunawapa utaalamu kwanini tunawasaidia hawa watoto Kwa sababu hawa ni Victim wa udhalilishaji ukiangalia mtoto anaekinzana na sheria utagundua kuwa nae kadhalilishwa Kwa namna Moja au nyengine", amesema wakili huyo.

Mohammed Khamis Faki, mkaazi wa Kazole anaemlea mtoto wa dada yake  ajulikanae Kwa jina Khamis Mwadini Kheir mwenye umri wa  miaka 16 alishtumiwa Kwa kosa la kukashifu mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 16 mnamo mwezi wa march 2023 huko maeneo ya Daraja bovu wilaya ya maghari A unguja.

Katika shitaka hilo lililopekea kufikishwa kituo Cha polisi Mwera na kesi kupelekwa mahakamani Vuga mjini unguja, ndugu Mohd Khamis amesema baada ya kufikishwa mahakamani shtaka la mjomba wake awali walishindwa Kwa Kukosa wakili kutokana na hali yao ya kimaisha.

"Tulipandishwa mahakamani Vuga tulishindwa kupata wakili kutokana na hali zetu ndipo tukaunganishwa na Mtu kwenye hili shirika hili pale mikunguni linalosaidia watu wasio na uwezo na Kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu Lile shirika lilitusaidia mpaka kesi ilipomalizika na alhamdullillah hatukutozwa  ushuru wowote ule", ameongeza

Amesema msaada walioupata kutoka shirika la ZALHO ni mkubwa kwani walishindwa na fedha za kuwapa wakili ili kuwasaidia kesi ya mjomba wake na Kwa Sasa mjomba wake huyo yupo huru na amejifunza kutokana na kosa Lile pamoja na kimkataza kufika katika mtaa aliopatia mtihani huo.

"Kwa Sasa tumempiga Marufuku kufika mitaa ya Daraja bovu ambako ndipo alipo huyo binty kwenye hiyo nyumba aliofika mjomba wangu na kwa sasa hata hasogei kwani ulikuwa ni mtihani tu ule kwake" Amesema.

Wizara ya Màendeleo ya Jamií, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar imesema hali ya upatikanaji huduma kisheria Kwa watoto ni ndogo na ndio maana wameona Kuna haja ya kutia mkono sheria iliopo Sasa ili kuboreshwa Kwa huduma.

Mkuu wa Division ya hifadhi ya mtoto katika Idara ya Ustawi wa Jamii na Wazee, Sheikh Ali Sheikh amesema watoto wanaokizana na sheria sheria bado inamtanzama kama mtoto mbali ya kuwa wanatenda makosa lakini sheria inataka kuwalinda pia na kupewa haki zao.

Amesema kama idara inatoa msaada wa kisheria Kwa kuwasimamia mahakamani hadi pale hukumu zinapotokea ambazo kikawaida ni kutozwa faini tu na sio kufungwa baadae idara inawapeleka vituo vya kurekebisha tabia kwenda kupata ujunzi na kujiweka sawa.

"Tunamsaidia kama mtoto kama sheria inavyotaka atizamwe Kwa hiyo Kuna maafisa wetu mahakamani kuhakikisha juu ya kesi zao kama watenda makosa lakini mwisho wa siku Sheria inataka iwalinde" amesema.

Kwa mujibu wa Wizara taasisi za usaidizi wa sheria, waratibu na wadau mbali mbali mbali, suala la usaidizi wa sheria linahitaji kupewa kipaumbele Zaid huku wazazi nao wakitakiwa kusimamia msingi mzima wa malezi Kwa watoto wao ili kupatikana kizazi chenye maadili mazuri.

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango