NBC kushirikiana na taasisi SMZ kukusanya mapato, kuimarisha huduma
NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Dk. Saada Mkuya Salum (pichani), amesema mashirikiano kati ya benki ya taifa ya biashara (NBC) na taasisi za Serikali kwenye matumizi ya mifumo ya kidigitali yataongeza ufanisi kwa taasisi za serikali hususani katika ukusanyaji wa mapato.
Alieleza kuwa hatua hiyo pia itachochea upatikanaji wa huduma bora kwa wateja na kuondoa urasimu unaochochea vitendo vya upotevu wa mapato lakini pia kukuza uwekezaji nchini.
Aidha alieleza kuwa serikali inakamilisha maandalizi ya sheria ya serikali mtandao ili kuipa nguvu tasisi hiyo kuwa mamlaka badala ya wakala ili iweze kusimamia vyema utekelezaji wa mkakati wa serikali mtandao.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi, alieleza kuwa makubaliano hayo yanalenga kuimarisha azma ya serikali kuziba mianya ya upotevu wa mapato yatokanayo na malipo ya ada na maduhuli mbali mbali lakini pia kuchochea biashara.
Alisema pande zote mbili zinatarajiwa kunufaika katika maeneo mbali mbali yakiwemo ya uwekaji wa kumbukumbu, kuimarisha biashara na uchumi pamoja na huduma zinazotolewa na taasisi hiuzo pamoja na benki hiyo.
Aidha Sabi alisema utiaji saini huo ni mwendelezo wa utekelezaji wa mipango ya benki hiyo kuimarisha huduma kwa wateja wake kupitia matawi waliyonayo Zanzibar, mawakala zaidi ya 200 na kupitia mitandao ya intaneti ambapo mteja anaweza kufanya malipo ya huduma za taasisi walizosaini nazo makubaliano kupitia mfumo wa Zan Malipo kwa urahisi zaidi.
Kwa upande wao, viongozi wa taasisi ziliizosaini makubaliano hayo, walisema mkataba huo utawawezesha kuimarisha utendaji wa kazi zao ikiwa pamoja na kujua hali ya kifedha ya taasisi zao hivyo kutoa huduma bora kwa umma.
Nae Meneja Fedha wa
Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), Riziki Faki, aliipongeza benki ya NBC kwa
kuingia makubaliano nao akiamini kuwa hatua hiyo itanusuru upotevu wa mapato na
kuondoa wasiwasi wa watendaji wao wanaposafirisha fedha kutoka vituoni.
Taasisi zilizoingia makubaliano hayo yaliyoshuhudiwa na Dk. Mkuya ni mbali ya ZBS na ZECO ni Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), Idara ya Ushirikiano kati ya serikali na Sekta binafsi (ZPPP), Mamlaka ya Ukuzaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF).
Comments
Post a Comment