Nsokolo ahimiza ulinzi wa waandishi, vyombo vya habari
NA KHAMISHUU ABDALLAH
RAIS wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), DeogratIus Nsokolo, amewasisitiza waandishi wa habari kuuelimisha umma juu ya umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari na nafasi ya waandishi katika jamii.
Nsokolo alitoa rai hiyo
wakati akifungua mdahalo kuadhimisha siku ya kimataifa ya Kukomesha Uhalifu
dhidi ya Waandishi wa Habari uliofanyika wa njia ya mtandao jana, ulioshirikisha
waandishi wa habari, viongozi wa klabu za wanahabari, UTPC na wadau wengine.
Alisema hatua hiyo
itasaidia kuongeza ufahamu kwa jamii jinsi vyombo vya habari vinavyochangia
kujenga jamii yenye habari na taarifa sahihi na uelewa utakaoujenga
mazingira bora kwa wanahabari kufanya kazi zao bila ya vitisho na vikwazo.
Aidha alisema pia
hatua hiyo inaweza kuzuia misimamo ya upande mmoja na kupotosha habari kwa
kuuelimisha umma jinsi waandishi wanavyochunguza na kuripoti masuala yanayowahusu
na vitendo visivyo na maadili.
Aliongeza kuwa ili
kujenga taifa lenye umoja, mshikamano na amani, vyombo vya Habari vinapaswa
kuripoti mambo kwa usawa hivyo vinapaswa kuachwa kufanya kazi zake kwa
kuzingatia weledi.
alisema umma
ulioelimishwa unaweza kushiriki zaidi katika mchakato wa kisiasa na
kijamii hivyo kuwa na mchango mkubwa katika ujenzi wa taifa.
Akizungumzia
maadhimisho ya siku hiyo yanayofanyika kila Novemba 2 ya kila mwaka, alisema yamelenga
kuongeza uelewa kuhusu changamoto zinazowakabili wanahabari katika utekelezaji
wa majukumu yao na hatua za kuchuku kuondoa vitisho na madhila juu yao.
Alisema waandishi
wa habari wamekuwa wakishambuliwa, vyombo vya habari kuwekewa vikwazo, matumizi
na taratibu za kimahakama dhidi ya waandishi wa habari kutokana na kazi
zao za uandishi wa habari zenye maslahi kwa umma.
Aidha aliupongeza Ubalozi
wa Uswizi nchini Tanzania, Jeshi la Polisi Tanzania, Baraza la Habari Tanzania
(MCT) na wadau wengine kwa kushirikiana na UTPC kuhakikisha usalama wa
waandishi wa habari nchini kuwawezesha kuendelea kutimiza majukumu yao kwa mujibu
na sheria za nchi.
Wakichangia katika
mdahalo huo, waandishi wa habari na viongozi wa Klabu walisisitiza haja ya
kuimarishwa mshikamano miongoni mwa wanahabari na taasisi wanazofanyia kazi ili
kupunguza uwezekano wa kujiweka kwenye hatari.
Walieleza kuwa
pamoja na baadhi ya maeneo kutokabiliwa na vitisho au madhila mara kwa mara,
bado waandishi wengi wanafanya kazi katika mazingira hatarishi yanayochangia
kutozingatia misingi ya taaluma yao.
Walisema kuwa hali
hiyo inatokana na waandishi wengi kufanya kazi bila ya mikataba ya ajira au
malipo ya uhakikia na kushauri kutanuliwa kwa wigo wa mijadala juu ya usalama
wa waandishi kwa kuwajumuisha wadau zaidi ya vyombo vya ulinzi na usalama,
waajiri na wamiliki wa vyombo vya habari.
Hata hivyo
walishauri kuimarishwa kwa sheria za habari Tanzania bara na Zanzibar ili zitoe
ulinzi kwa waandishi na vyombo vya habari ambao pia wamehimizana pia kujitambua
na kusimamia maadili ya taaluma yao.
Akifunga mdahalo
huo, Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC, Kenneth Simbaya, aliwahimiza wanahabari
kuendelea kupaza sauti juu ya madhila wanayopitia ili kupata njia ya
kuyapunguza.
Alieleza kuwa UTPC kwa
kushirikiana na wadau wengine wanaendelea kutafuta njia zitakazosaidia kujenga
uwezo wa mwaandishi na wadaiu wengine ili kupunguza matukio ya uvunjifu wa uhuru
wa kujieleza ambao ni sehemu ya haki za binadamu.
Kwa mujibu wa Shirika
la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO), waandishi wa habari
117 waliuawa mwaka 2021/2022 ambapo asilimai 38 walitoka katika mabara ya Latini
Amerika na Asia huku asilimia 14 ya kesi za uhalifu dhidi ya waandishi wa habari
zikiendelea kushughulikiwa.
Comments
Post a Comment