Vodacom yawapa uhakika wa matibabu mama, watoto wachanga

NA MWANDISHI WETU

KAMPUNI ya mawasiliano ya Vodacom imetoa zawadi ya bima kubwa ya afya kwa mama 100 na watoto wachanga 100 waliozaliwa na kulazwa katika hospitali ya rufaa ya Mnazimmoja, Zanzibar.


Mama (mzazi)  Maryam Yohana Daniel (aliyeketi) akipokea bima kubwa ya afya kwa niaba ya wenzake wakati wa hafla ya ugawaji wa bima hizo kwa mama wazazi na watoto katika hospitali ya Mnazimmoja.

Hatua hiyo ni sehamu ya kampeni ya kampuni hiyo ya kueneza upendo katika msimu wa sikukuu ambapo kina mama waliojifungua kuanzia Novemba 9, mwaka huu katika hospitali hiyo watapatiwa bima ya ‘Voda Bima’.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi bima hizo, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Annette Kanora (wa tatu kushoto), alisema hatua hiyo ni muendelezo wa mpango wa kampuni hiyo kuwashukuru wateja wake na kusaidia kupunguza changamoto zinazoikabili jamii.

 Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Annette Kanora (wa tatu kushoto) pamoja na watendaji wa Vodacom Tanzania wakizungumza na baadhi ya wauguzi wa wadi ya wazazi

“Kwa mwaka huu tumeona umuhimu wa kuifikia jamii pana zaidi kwani tunajua mama wanaojifungua hukabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za matunzo ya watoto hivyo bima hii inakwenda kusimamia huduma zote za kiafya kwa mama na mtoto”, alieleza Annette.

Alifafanua kuwa faraja hiyo itawafikia wazazi wa maeneo mbali mbali nchini na kwamba kampuni hiyo imelenga kuwafikia mama wazazi 1,000 na watoto wachanga 1,000 ambapo kwa Zanzibar kinamama 100 na watoto wao watapata huduma za matibabu katika hospitali ya Ampola (Global), Tawakal, Al Rahma na Mnazimmoja pamoja na Muimbili na nyengine za Tanzania bara. 


Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Annette Kanora, akimbeba mmoja ya watoto mapacha wa mama Badria Mohamed Khamis. 

Akizungumzia kuhusu kampeni ya ‘Sambaza Shangwe, Gusa Maisha’ Meneja Mauzo Vodacom Zanzibar, Fadhili Linga, alisema kampeni hiyo inatoa zawadi kwa wateja wao lakini pia kutoa misaada ya kijamii kama hiyo.

Linga alisema sekta ya afya ni eneo muhimu na kampuni hiyo imeona iunge mkono juhudi za serikali kupitia miradi mbali mbali inayoendeshwa na kampuni hiyo ukiwemo wa M - Mama.

Aidha aliahidi kuwa wataendeleza ushirikiano uliopo kati yao na serikali zote mbili za Tanzania ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa Watanzania.


Maofisa wa Vodacom Tanzania akiwemo Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Annette Kanora (wa tatu kulia) na bwana shangwe wakiwa na mama mzazi Maryam Yonane Daniel 

“Mbali na kutoa bima ya afya, Vodacom inatoa zawadi za bodaboda, TV, simu za mkononi, ‘router’ za intaneti ya 4G na 5G lakini pia pesa taslimu kuanzia shilingi 500,000 hadi 10,000,000 kwa lengo la kuinua uchumi wa watanzania”, alieleza Meneja huyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wodi ya Wazazi hospitali ya Rufaa Mmnazimmoja, Khadija Salum Said, aliipongeza kampuni hiyo kwa ubunifu wa kampeni hiyo ambayo inawajali kinamama wanaoleta viumbe wapya duniani.

Alisema bima hizo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa huduma ya uhakika ya afya ya mama na mtoto wakati wa hatua ya awali wa makuzi ya watoto wachanga na akina mama waliotoka kujifungua ili kupunguza vifo vya mama na watoto wachanga.

“Kuwapatia bima ya afya tena ile kubwa kwa mwaka mzima kunawondolea hofu na shaka pindi watakapokua na changamoto za kiafya na kupunguza matatizo yatayotokea baada ya mama kujifungua na hata kupunguza vifo vya watoto wachanga”, alisema.

Wakizungumza kwa niaba ya wazazi wenzao waliopatiwa bima hizo Maryam Yohana Daniel na Badria Mohammed Khamis aliyejifungua watoto mapacha wa kike, walipongeza uamuzi wa kampuni hiyo na kueleza kuwa bima hizo zitawasaidia kupata matibabu kwao na watoto wao na huduma nyengine za kiafya.

Hivyo waliiomba jamii kuendelea kuiunga mkono kampuni hiyo ili iweze kutoa msaada kwa watu wengi zaidi ya Watanzania ambapo kupitia ‘Voda Bima’ watawawezesha akina mama na watoto wao kupata huduma za afya ikiwa ni sehemu ya kampeni inayoendelea ya ‘Sambaza Shangwe, Gusa Maisha’.

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango