Wadau TIB watakiwa kuimarisha mashirikiano

NA MWANDISHI WETU 

WADAU wa Benki ya Maendeleo nchini (TIB) wametakiwa kuimarisha mashirikiano ili kuongeza mchango wa benki hiyo katika maendeleo ya taifa.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila (kushoto) akisalimiana na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Maendeleo TIB, Agapiti Kobello (wapili kushoto) wakati alipowasili kufungua Mkutano wa Wadau wa Benki ya Maendeleo (TIB) Kanda ya Dar es Salaam uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam. Wengine ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa TIB, Juma Hassan Reli (watatu kushoto), Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TIB, Lilian Mbassy (wapili kulia) na Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa Miradi, Zuwena Hemed (kulia). 

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Albert Chalamila wakati akifungua mkutano wa majadiliano uliowakutanisha watendaji na wadau wa benki hiyo wa kanda ya Dar es salaam ulioangalia majukumu na mafanikio ya benki hiyo katika kuchangia maendeleo nchini.

Mkutano huo pia uliangalia fursa za mikopo na huduma zinazotolewa na TIB lakini pia  na kupata mrejesho kutoka kwa wadau utakaoiwezesha benki hiyo kuimarisha huduma zinazotolewa na benki.   

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila (wapili kushoto waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wadau wa Benki ya Maendeleo (TIB) (waliosimama) mara baada ya kufungua Mkutano wa Wadau wa Benki ya Maendeleo TIB – Kanda ya Dar es salaam uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es salaam. Wengine pichani waliokaa ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi (TIB), Agapiti Kobello (kushoto), Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa (TIB), Lilian Mbassy (wapili kulia) na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo Juma Reli (kulia). 

 Aidha Chalamila aliipongeza TIB kwa kuwezesha miradi ya uwekezaji hali inayochangia na kuimarisha shughuli za maendeleo sambamba na ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na nchi kwa ujumla. 

“Nawapongeza kwa kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 110.40 kwa miradi iliyo kwenye kanda ya Dar es salaam ambapo kati ya fedha hizo zinagharamia miradi ya uwekezaji wa zaidi ya shilingi bilioni 900 zilizowekezwa na TIB”, alisema Chalamila. 

Aidha Chalamila alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya uwekezaji katika benki hiyo kwa kuwa ina mkono wa serikali na uamuzi wa kuiimarisha unadhihirisha mapenzi aliyonayo kwa benki hiyo. 

"Kuendelea kukua kwa Benki hiyo kunatanua fursa za ajira kwa vijana wa kitanzania ambao wajipatia kipato na kuchangia katika kukuza uchumi wa Taifa," aliongeza Chalamila. 

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo, Mjumbe wa Bodi, Agapiti Kobello, alisena TIB itaendelea kukutana na wadau wake mara kwa mara kupata mrejesho wa huduma wanazowapatia ili kuimarisha utendaji wa kazi.

Alieleza kuwa kufanya hivyo ni kutekeleza mkataba kati ya Msajili wa Hazina na Bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo unaoweka vigezo kwa taasisi za fedha kuhusu huduma kwa wateja. 

“Mkataba wa utekelezaji kati ya Msajili wa Hazina na Bodi ya Wakurugenzi wa Benki yetu umeweka kiwango cha asilimia 15 katika kipengele cha huduma kwa mteja kupima uwezo wa taasisi katika kutoa huduma bora na za kiubunifu kwa wateja wake, ikiwa ni pamoja na kukua kwa idadi ya wateja”, alisema Kobello. 

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TIB, Lilian Mbassy, alieleza kuwa mchango wa uwekezaji uliofanywa na benki hiyo nchini umewezesha miradi katika sekta mbalimbali iliyotoa ajira zaidi ya 30,000 kwa Watanzania. 

Aidha Mbassy alisema TIB kama benki ya kisera itaendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kutekeleza sera na mikakati  ya kitaifa ili kuongeza kasi ya maendeleo hapa nchini. 

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango