Balozi Mpanda ahimiza ubunifu uhifadhi wa mazingira

JUVIEKA, wadau wapanda mikoko 2,540 Mtopwani

NA MWANDISHI WETU

JUMLA ya miche ya miti ya mikoko 2,540 imepandwa katika eneo la Mdodo madema, Shehia ya Mto wa pwani mkoa wa Kaskazini Unguja ili kutunza mazingira ya eneo hilo.


Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mratibu wa zoezi hilo ambaye ni kiongozi wa Jumuiya ya Vijana ya Uhifadhi wa Mazingira, Mbarouk Maalum, alieleza kuwa zoezi hilo lililofanyika jumapili iliyopita lilihudhuriwa na wanaharakati wa mazingira 117 kutoka taasisi na makundi mbali mbali ya jamii.

Aliongeza kuwa miongoni mwa washiriki hao ni vikundi vitano vya wanufaika wa mpango wa MKUBA, wanachama na viongozi wa mabaraza ya vijana ya Shehia za Mtowapwani na Chutama,  wawakilishi taasisi za JUVIEKA, UNA, ZAFELA pamoja na Sheha wa Shehia hiyo na wananchi wake.

Aidha maalum alieleza kuwa shughuli hiyo pia ilihudhuriwa na Balozi wa mazingira kutoka ofisi ya rais, Muungano na Mazingira ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Khadija Yussuph Mpanda ambaye pia ni miongoni mwa wanahrakati wanaounga kundi la Green Samia ilidhihirisha utayari na ushiriki wa jamii na wadau katika vita dhidi ya uharibifu wa mazingira.

Aliongeza kuwa zoezi hilo limejenga uelewa kuhusu umuhimu wa kupanda miti, kutambua na kupeana habari za mazingira na wadau kuoneshana fursa zinazoweza kuleta manufaa huku akiainisha kuwa uelewa mdogo wa jamii juu ya umuhimu wa kupandaji miti na upungufu wa mbegu za mikoko kuwa ni miongoni mwa changamoto walizobiliana nazo.

“Napenda kuwashukuru wale wote ambao Allah aliwawezesha kufika na hata wale ambao hawakujaaliwa kupata nafasi ya kuja kutokana na sababu za hapa na pale katika zoezi la upandaji wa mikoko katika eneo hili ikiwa ni njia moja wapo ya kulihifadhi ili maji ya bahari yasiliharibu”, alieleza Maalum.

Akizungumza baada ya kushiriki zoezi hilo na alipokutana na wanachama wa klabu ya waandishi wa Habari Zanzibar katika ofisi za klabu hiyo kijangwani jumamosi iliyopita, Balozi Khadija Mpanda, alieleza haja ya jamii kujengewa uelewa juu ya namna bora na endelevu ya uhifadhi wa mazingira ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Alieleza kuwa nchi za visiwa kama Zanzibar zimeaathiriwa zaidi na shughuli za kibinadamu hivyo ubunifu na mikakati endelevu inahitajika kuzuia madhara yanayotokana na uharibifu wa mazingira na nchi kavu na baharini.

Alifafanua na kupongeza juhudi zinazochukuliwa na wadau mbali mbali zanzibat katika harakati za kutunza na kuhifadhi mazingira kwa kusafisha na kutumia vifaa chakavu vinavyorejesheka kutengenezea vitu vinavyoweza kutumika kwa manufaa ya jamii na kuzalisha kipato.

Aidha aliviomba vyombo vya Habari, kujielekeza katika elimu juu ya mazingira kwa kuwasaidia vijana wenye bunifu zinazotoa suluhisho la kukabili athari za mabadiliko ya tabia nchi kuonesha bunifu zao ili kujenga utayari wa jamii kuzitumia taka ngumu na nyenginezo kama fursa ya kujipatia kipato.

Balozi khadija aliyekuwepo Zanzibar kwa ajili ya sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi, alitumia ujio wake kutembelea maeneo na kushiriki vikao na shughuli zinazohusiana na ulinzi, uhifadhi na utunzaji wa mazingira na kupongeza hatua za maendeleo zilizofikiwa.



Comments

Popular posts from this blog

ZAMECO yakerwa na video ya udhalilishaji mtandaoni