Mkakati, mpango kazi kuimarisha mianzi wazinduliwa
NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki, amezindua mkakati wa uimarishaji wa miti ya mianzi na kueleza kuwa tafiti zimebaini kuwepo kwa takribani hekta milioni 12.5 zinaweza kuuteshwa miti hiyo nchini ili kuzuia mmomonyoko wa ardhi na kunyonya hewa ukaa.
Amesema utafiti huo unaonesha Tanzania inapoteza eneo la misitu yenye ukubwa wa hekta zaidi la 469,000 kila mwaka, hali ambayo sio nzuri na halikubaliki hivyo juhudi za pamoja zinahitajika.
Kairuki alieleza hayo jana wakati akizindua mkakati wa kitaifa wa mianzi na mpango kazi wa mkakati huo uliofanyika katika Chuo cha Taifa cha Utalii, Dar es salaam.
Alisema miti ya mianzi ina nafasi kubwa katika uhifadhi wa mazingira kwa kufyonza hewa ya ukaa (carbondioxide) kwa zaidi ya mara 40, hivyo zao hilo ni muhimu katika utunzaji wa mazingira na kupunguza athari za mabadiliko ya Tabianchi.
WAZIRI Kairuki akiwa na Katibu Mkuu Abbas, Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya bunge ya Ardhi, Maliasili na Utali - Timotheo Mnzava (kulia) na Mwakilishi wa Mkuu wa mkoa wa Dar es salam.
Alieleza kuwa mkakati huo wa mwaka 2023 - 2031, ambao wenye kauli mbiu ‘Tanzania inawekeza katika Mianzi kwa ajili ya uhimilivu na kuwa na uchumi endelevu’ unalenga kuimarisha uchumi na wananchi kuweza kupata kipato kutokana na manufaa yaliyopo katika mianzi.
WAZIRI wa Maliasili
na Utalii, Angellah Kairuki, akikabidhi mkakati wa kitaifa wa mianzi na mpango
kazi wake kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na
Utalii, Timotheo Mnzava mara baada ya kuuzindua.
Aidha aliongeza kuwa Idara ya Misitu na Nyuki imekasimiwa kuwa dhamana wa sera, sheria, kanuni na miongozo kwa namna ambavyo wanaweza kuratibu vyema kazi, pamoja na kulishukuru Shirika la kimataifa la Mianzi Duniani (INBAR) kwa kuwapa ushauri wa kitaalamu na ufadhili wa kifedha katika uandaaji wa mkakati huo.
MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la kimataifa la Mianzi Duniani, Balozi Ally Mchumo, akipokea kitabu cha mkakati wa kitaifa na mpango kazi wa uimarishaji wa miti ya mianzi toka kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki mara baada ya kuuzindua.
Nae Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Mianzi Duniani, Balozi Ally Machumo alisema mianzi inasaidia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuzuia matumizi ya plastiki.
Alieleza kuwa mti huo unaweza kutengenezwa bidhaa mbali mbali vikiwemo vifaa vya matumizi ya nyumbani kama vikombe na vitu vyengine.
“Mwakani kutakuwa na mkutano wa kimataifa wa mianzi wa Afrika nchini Tanzania, hivyo mkakati huu umekuja wakati muafaka katika kukuza zao la mianzi nchini ambapo Tanzania ilikuwa nchi wanachama tokea mwaka 1997 lilipoanza utafiti wake”, alieleza Balozi Machumu.
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki (kulia), akimkabidhi Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Hassan Abbas, mkakati wa kitaifa wa mianzi na mpango kazi wa mkakati huo mara baada ya kuuzindua hafla iliyofanyika katika Chuo cha Taifa cha Utalii, Dar es salaam.
Mapema Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili
na Utalii, Dk. Hassan Abass alisema mianzi inapopandwa katika eneo la makaazi inasaidia
kuweka hewa mzuri na kuleta furaha na baraka katika nyumba pamoja.
Akizungumza na wandishi wa
habari, Kamishna wa wakala wa misiti nchini (TFS), Prof. Dos Santos Silayo,
alisema mkakati huo utaifanya Tanzania kuwa sehemu ya nchi 50 duniani wanachama
wa shirika la kimataifa la mianzzi kutumia miti hiyo kama mmea wa faida.
Comments
Post a Comment