Wadau uwindaji kitalii wachangia miradi ya maendeleo
NA MWANDISHI WETU, ARUSHA
UWINDAJI wa kitalii
umechangia kiasi cha Dola 2,546,295 za Marekani sawa na Shilingi bilioni 6,606,635,525
ndani ya kipindi cha 2020/2021 na 2022/2023.
Fedha hizo zimetolewa kwenye miradi mbali mbali ya maendeleo na uendelezaji na shughuli za uhifadhi kwenye Maeneo ya Hifadhi za Wanyamapori za Jamii (WMA).
Naibu Waziri wa
Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula, alieleza hayo alipokuwa anafungua
warsha ya wadau wa uhifadhi wa mnyama tembo kwenye mifumo ya ikolojia inayovuka
mipaka ya nchi jijini Arusha.
Aidha Kitandula
alisema kuwa pamoja na mchango mkubwa unaotolewa na uwindaji wa kitalii kwenye
mifumo ikolojia inayovuka mipaka ya nchi, ipo haja ya kuchanganua changamoto za
matumizi ya wanyamapori hao zinazochangiwa na wanyama hao kupatikana katika
mifumo ya ikolojia inayovuka mipaka ya nchi hivyo tembo hutoka nchi moja kwenda
nchi nyingine.
Kitandula aliongeza
kuwa katika warsha hiyo anategemea kuwa wadau mbalimbali wa uhifadhi watapata
fursa ya kujadiliana changamoto hizo, kupeana uzoefu na mwisho watatoka na
majibu ya namna bora ya kutatua changamoto zinazotokana na usimamizi wa mnyama
tembo kwenye mifumo ikolojia iliyohifadhiwa ambayo inavuka mipaka nchi.
“Lengo ni
kuhakikisha kuwa uwindaji wa tembo unafaidisha jamii lakini pia unachangia
katika uhifadhi na uchumi wa Taifa kwa ujumla kupitia maandalizi miongozo na
kanuni zitakazowezesha uwindaji wa tembo kwa maendeleo na uhifadhi”, alisema Kitandula.
Vilevile Kitandula
kwa niaba ya Waziri wa Maliasili, Angela Kairuki alimpongeza na Raisi wa
taasisi ya Conservation Force (CF) John Jackson, kwa juhudi kubwa alizofanya
katika kusaidia uhifadhi wa mnyama tembo kupitia uwindaji wa kitalii lakini pia
kusaidia Tanzania katika utekelezaji wa Mkataba wa Kimataifa wa Biashara
ya Wanyamapori na mimea iliyo hatarini kutoweka (CITES) na kupambana
biashara haramu ya nyara nchini Marekani.
Comments
Post a Comment