‘Uchaguzi serikali za mitaa kuzingatia falsafa ya 4R’
NA SAIDA ISSA, DODOMA
IMEELEZWA kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024 utazingatia maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan kama ambavyo amekuwa akizungumza katika majukwaa mbali mbali akisisitiza falsafa ya ‘4R’ kwa maana ya maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na kujenga upya.
Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Rais,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Festo Dugange, katika kikao
cha viongozi wa dini, Asasi za Kiraia na Mashirika yasiyo ya Kiserikali kujadili
rasimu ya kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024.
Ambapo alisema kuwa uchaguzi huo utazingatia maono hayo ya
Mheshmiwa Rais ili kila chama kipate nafasi sawa katika uchaguzi.
"Ndugu washiriki, rasimu za kanuni zilizoandaliwa ni
kama ifuatavyo, Rasimu ya Kanuni za Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kijiji, Wajumbe
wa Halmashauri ya Kijiji na Mwenyekiti wa Kitongoji katika Mamlaka za Wilaya za
Mwaka 2024”, alieleza.
Aliongeza kuwa; “Rasimu ya Kanuni za Uchaguzi wa Mwenyekiti
wa Mtaa na Wajumbe wa Kamati ya Mtaa katika Mamlaka za Miji za Mwaka, 2024, Rasimu
ya Kanuni za Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kijiji, Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji
na Mwenyekiti wa Kitongoji katika Mamlaka za Miji za Mwaka, 2024 naRasimu ya
Kanuni za Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kitongoji katika Mamlaka za Miji Midogo za
Mwaka, 2024".
Aidha Naibu huyo alisema kuwa lengo la kikao jicho ni kwa
ajili ya kupitia rasimu za Kanuni zilizoandaliwa na kutoa maoni yao kwa lengo
la kuboresha.
"Ni matumaini yangu kuwa kila mmoja wenu atashiriki
kikamilifu na kutumia muda vizuri katika kutoa michango chanya itakayosaidia
kuboresha rasimu zilizoandaliwa, Ninapenda kuwashukuru tena kwa ushirikiano
wenu na kujitoa kwenu katika kutekeleza shughuli nyingine za maendeleo pamoja
na kusaidia jamii,"alisema.
Kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya)
Sura 287 na Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Sura 288, uchaguzi wa
viongozi wa Serikali za Mitaa hufanyika kila baada ya miaka mitano (5). Kwa
kuwa uchaguzi wa mwisho ulifanyika Novemba, 2019, uchaguzi unaofuata utafanyika
Novemba, 2024.
Sheria ya Serikali za Mitaa zinampa Mamlaka Waziri Mwenye
Dhamana na Serikali za Mitaa kuandaa Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
kwa ajili ya kusimamia uchaguzi husika na Kanuni hizo zitawasilishwa kwenu kwa
ajili ya kupata maoni.
Aidha, rasimu ya kanuni mtakazozipitia leo zimezingatia
michango na maoni ambayo yamekuwa yakiwasilishwa na wadau mbalimbali wakiwemo
viongozi wa vyama vya siasa kiwemo suala la mgombea kutopita bila kupingwa na
Wakurugenzi wa Halmashauri kutosimamia uchaguzi.
"Ndugu washiriki, ninapenda kuwakumbusha kuwa, Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limetunga Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya
Uchaguzi ya mwaka 2024 na Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya
mwaka 2024”, alieleza.
“Aidha, Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya
mwaka 2024 imefuta sheria ya Taifa ya Uchaguzi ya mwaka 1985 na sheria ya
uchaguzi wa Madiwani ya Serikali za Mitaa ya Mwaka 1976", alisema.
Alisema kuwa Marekebisho yaliyofanyika yamezingatia pia maoni
ambayo yamekuwa yakitolewa na wadau ikiwemo suala la namna ya kumpata kiongozi
pale anapokuwa mkombea mmoja.
"Kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa huandaliwa ili
kukidhi matakwa ya kifungu 201A cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za
Wilaya) Sura 287 na kifungu 87A cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za
Miji) Sura 288 vinavyomtaka Waziri mwenye dhamana na serikali za mitaa kuweka
utaratibu wa uchaguzi wa serikali za mitaa kupitia Kanuni, kwa kuzingatia kuwa,
vyama vya siasa ni wadau muhimu katika uchaguzi wa cerikali za mitaa, maoni
yenu ni muhimu ili kuboresha kanuni zilizoandaliwa", alisema.
"Aidha ushiriki wenu katika maandalizi ya kanuni hizi ni
maelekezo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia
Suluhu Hassan ambaye anataka uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Mwaka 2024 kuwa
huru na haki", alifafanua.
Comments
Post a Comment