Mifumo ulinzi mali za serikali kuimarisha uchumi

NA MWANDISHI WETU

NAIBU Katibu Mkuu Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Dk. Mzee Suleiman Mndewa, amesema hatua ya kuimarisha uchumi wa kidigitali, itafikiwa endapo watumishi wa umma watatumia mifumo itakayosaidia mali za serikali kubaki salama.

Naibu huyo, amesema hayo Julai 15, 2024 alipofungua mafunzo kwa watendaji wa taasisi sehemu ya IT, wahasibu, wakaguzi wa ndani na wasimamizi wa mali za serikali, juu ya matumizi ya mifumo katika kurikodi mali za serikali yaliofanyika katika hoteli ya Golden Tulip, Uwanja wa ndege Zanzibar.

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk. Mzee Suleiman Mdewa, akifungua mafunzo ya usimamizi wa mali za umma kwa njia ya kidigitali yaliowashirikisha maofisa TEHAMA na wasimamizi wa mali za umma wa Serikali.

Amesema mfumo wa udhibiti wa mali za serikali ni muhimu katika uchumi wa kidigitali, kwani utakapotumika vizuri utairahisisha kufanyika maamuzi kwa urahisi huku ikiwa na vielelezo vya ushahidi wa uhakika na gharama nafuu.

Amefafanua kuwa hatua hiyo, itaisaidia serikali kujua usalama wa mali zake na sehemu zilipo, kwani hivi sasa kuna changamoto ya baadhi ya taasisi kushindwa kuzidhibiti kutokana na utaratibu unaotumika sio rafiki kwa serikali.

“Tunashirikiana kwa pamoja kufikia maono ya maendeleo ya taifa 2025 na kuendeleza uchumi wetu wa kidigitali kupitia uanzishaji wa mfumo wa taarifa za usimamizi wa mali za serikali ya Zanzibar, mfumo huu unalenga kuboresha jinsi tunavyosimamia mali za umma na kuongeza ufanisi kwa jumla”, amesema Mndewa.

Ameongeza kuwa hivi sasa serikali imejitolea kutumia teknologia za kidigitali kwa maendeleo ya Zanzibar, kwa lengo kutekeleza mkakati wa dira ya maendeleo wa kufikia mwaka 2050.

BAADHI ya washiriki wa mafunzo ya usimamizi wa mali za umma kwa njia ya kidigitali yaliowashirikisha maofisa TEHAMA na wasimamizi wa mali za umma wa Serikali wakifuatilia uwasilishaji mada.

Amesema sera hiyo, itasaidia matumizi ya huduma za eletroniki kiuchumi kwa kuwa na usimamizi mzuri wa mali kwa kupata data kamili, kukidhi viwango na sheria, kumbukumbu za wazi na sahihi, kutambua na kufuatilia mali kuzuiya upotevu au wizi na kuhesabu kubadilika kuwa gharama za matengenezo na kuboresha raslimali.

Amewataka watendaji hao kuwasilisha taarifa kwa wakati katika mifumo, ili wazuiye uwepo wa ongezeko la gharama, kupugua kwa uzalishaji, hasara za kifedha, masuala ya kufuata sheria, kuvuruga operesheni, kufanya maamuzi mabaya na kuharibu sifa.

Nae, Msajili wa Hazina Zanzibar, Waheed Mohamed Ibrahim Sanya, amesema wameamua kutoa mafunzo hayo kwa watendaji wa Kada hizo, ili waisaidie serikali kuwa na utaratibu mzuri wa kulinda mali zake.

Msajili wa Hazina Zanzibar, Waheed Mohamed Ibrahim Sanya, akizungumza na waandishi wa habari kando ya mafunzo ya usimamizi wa mali za umma kwa njia ya kidigitali yaliowashirikisha maofisa TEHAMA na wasimamizi wa mali za umma wa Serikali.

Sanya (pichani) amesema kuwa utaratibu huo utasondoa ujanja uliokuwa ukitumika katika usalama wa mali za serikali, kwani mali hizo zitasajiliwa katika mfumo pamoja na kuzihakiki mali hizo.

Amesema hatua hizo zitafanyika ikiwa pamoja na kuwaandalia miongozo itayoyotumika kwa watendaji kujuwa wajibu wao, kwani mifumo hiyo itakuwa na kazi ya kutoa ripoti za utendaji kwa miezi mitatu ama sita na mwaka mmoja.

Nae Mwakilishi wa shirika la Umoja wa Maataifa, Uchumi na Masuala ya Kijamii (UNDESA), Daniel Platz, amesema wameamua kufanya mafunzo hayo yatayoisadia serikali kuzitambua changamoto zilizokuwa zikikumbana nazo na kuzisahihisha kwa wakati, kwa vile mifumo hiyo itazifanya mali za serikali kubaki salama.

Naye Aheid Talib, mmoj ya washiriki kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), amesema wanatarajia mafunzo hayo yatawawezesha kufanyakazi zao vizuri kwa vile tayari serikali inahitaji kwenda katika uchumi wa kidigitali, jambo ambalo linawahitaji utendaji wao kuwa na mabadiliko. 

Comments

Popular posts from this blog

Balozi Mpanda ahimiza ubunifu uhifadhi wa mazingira

Vodacom yawapa uhakika wa matibabu mama, watoto wachanga