Treni ya SGR ina faida kiuchumi, kijamii - RC Senyamule

NA SAIDA ISSA, DODOMA

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule (pichani), amesema usafiri wa treni ya kisasa una faida nyingi za kiuchumi na kijamii kwani utapunguza muda wa safari kutoka saa nane hadi tisa kwa usafiri wa mabasi hadi saa tatu na nusu kwa safari ya Dodoma – Dar es salam.

Hayo ameyaeleza Jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa rasmi wa safari za treni ya kisasa kwenda Morogoro – Dar es salaam kutokea Dodoma utakaofanyika Agosti 1, 2024 katika stendi kuu reli jijini Dodoma.

Senyamule amesema kuwa treni hiyo ya umeme itawawezesha wafanyabiashara kusafiri kutoka mkoa mmoja wa Dar es Salaam au Dodoma na kurudi kuendelea na biashara zao ndani ya muda mfupi.

"Kituo hiki cha treni kina sehemu mbali mbali ikiwemo sehemu zakufanyia biashara makundi, waje wafanyabiashara wanaotaka kufanyia biashara zao hapa, majengo ni ya kisasa, waje wawekeze kwani mkoa wa Dodoma ni mkoa wenye utalii, wageni watakao kuja na treni watajifunza na kuona vitu kwa kuanza na jengo la kituo cha treni wani ni kivutio tosha, vile vile zao la zabibu mbichi na kavu, vinywaji vinavyotokana zabibu na jinsi ya kutengeneza", amesema Senyamule.

Aidha amewataka wakazi wa Dodoma na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi katika uzinduzi rasmi wa safari za treni hiyo utakaofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan.

Uzinduzi huo unakuja baada ya kufaulu kwa majaribio ya safari za treni ya mwendo kasi kutoka Dar es salam hadi Morogoro na baadae Dodoma yaliyochukua zaidi ya miezi miwili ambapo kwa sasa safari za Dar es salam – Morogoro zinaendelea.

Comments

Popular posts from this blog

Balozi Mpanda ahimiza ubunifu uhifadhi wa mazingira

Vodacom yawapa uhakika wa matibabu mama, watoto wachanga