Jaji Mstaafu Luanda amrithi Jaji Mlay MCT
NA MWANDISHI MAALUM
MKUTANO Mkuu wa 26 wa wanachama wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), umemchagua Jaji Mstaafu Bernad Luanda (pichani) kuwa Rais wa baraza hilo kuziba nafasi iliyoachwa na jaji mstaafu Juxon Mlay, aliyefariki dunia mapema mwaka huu.
Akizungumza baada ya uchaguzi huo, Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Ernest Sungura, amewashukuru wanachama walioshiriki mkutano huo na kueleza kuwa baraza limejipanga kuimarisha huduma zake kwa wananchama ikiwemo kuwanoa waandishi wa habari.
Amesema, kuanzia mwaka ujao MCT itakua inatekeleza mradi mkubwa utakaojulikana kwa jina la ‘WAJIBIKA’ambao utakuwa wa miaka saba ambapo utakuwa na thamani ya pauni milioni 30, utakaogusa kila eneo, ikiwemo kuwajengea uwezo hata waandishi wa habari mmoja mmoja, kupiti vyombo vyao.
Alieleza kuwa, jingine ambalo litafanyika mwakani, ni sherehe kubwa na za aina yake, ya mafanikio ya ‘MCT’ kwa miaka 30, tokea lilipoanzishwa mwaka 1995.
Katibu Mtendaji huyo, aliwataka wanachama wenye madeni, ambayo kwa mwaka huu yamefikia shilingi milioni 167, kulipa haraka, ili kulipa uhai baraza hilo.
‘’Wanachama ambao wana deni la kufikia miaka 10, ni wengi na ndio maana, linafikia wastani wa shilingi milioni 167, fedha ambayo ingetusaidia, katika utendaji wa kazi zetu", alifafanua.
Aidha Sungura aliwapongeza waandishi wa habari kutoka maeneo mbali mbali ya tanzania kwa kujitokeza kwa wing na kuwasilisha kazi za kutafuta mshindi wa tunzo za uhamiri wa mwandishi wa habari Tanzania ‘EJAT’, mwaka 2023/2024.
Naye Makamu wa Rais wa MCT, Yussuf Khamis Yussuf, alisema anajivunia umoja na mshikamano, uliopo baina ya wanachama na watendaji wa MCT.
Hata hivyo, alisisitiza haja kwa wanachama wenye madeni, kusawazisha, ili kuona ‘MCT’ haitegemei mno fedha za wafadhili, katika kujiendesha kwake.
Akiwasilisha ripoti ya fedha, ya mwaka 2023, CPA Happiness Nkya, alisema taasisi hiyo iliingiza kiasi cha shilingi bilioni 1.1, ambapo ni upungufu wa shilingi milioni 600, ikilinganishwa na shilingi bilioni 1.6 za mwaka 2022.
Alieleza kuwa, kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 1.0 ni za wafadhili na shilingi milioni 38 ni michango ya ndani, ikiwemo ada ya mwanachama wa MCT.
Hata hivyo, alisema katika ukaguzi uliofanyiwa, wamepata hati safi, jambo linaloonesha kuendelea kufuatwa kwa taratibu za manunuzi na matumizi.
Baadhi ya wanachama akiwemo mwandishi Jabir Idrissa kutoka Zanzibar, alisema ujio wa baraza huru la habari la serikali, isiwe sababu ya MCT kujiondoa katika usimamizi wa weledi na ustawi wa vyombo vya habari.
‘’Hapa chakuzingatia tupate uzoefu katika baadhi ya nchi, kuona wanakwenda vipi, wanapokuwa na baraza la habari la serikali na lile binafsi kama MCT,’’alifafanua.
kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Keneth Simbaya, alimpongeza Katibu Mtendaji wa MCT kwa maono yake yanayoelekea kulivuusha baraza hilo.
Naye Issaya Kisibuli kutoka gazeti la Jibu la Maisha, aliomba wanachama ambao wanamadeni, kufuatiliwa kwa kina, ili waeleze sababu na misimamo yao.
Wakati huo huo, mkutano huo umewaidhinissha wanachama wapya kadhaa, ikiwemo blog ya Pemba Today, Bahari Media, Trust Media Agency, Pemba ya leo blog, Star TV na Redio free Afrika.
Comments
Post a Comment