Airtel Foundation yazindua mpango wa udhamini wa masomo kwa vijana
NA MWANDISHI WETU
KAMPUNI ya mawasiliano ya Aiirtel Tanzania imezindua mpango wa udhamini wa masomo katika fani za teknolojia kwa vijana wa Afrika wanaosoma katika taasisi ya teknolojia ya india (IIT – Madras) kampasi ya Zanzibar.
Uzinduzi huo umefanyika Oktoba 7, 2024 katika kampasi ya chuo hicho Bweleo, wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Dk. Dinesh Balsingh na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Muhamed Mussa.
Viongozi wengine ni Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Omar Kipanga, Balozi wa India nchini Tanzania, Dk. Biswadip Dey, Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Makame Machano Haji na Mkuruaenzi wa IITMZ Prof. Preeti Aghalayam.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Airtel Africa, Dk. Segun Ogunsanya, Dk. Dinesh amesema programu hiyo inahusisha wanafunzi wa Afrika walofaulu michipuo ya sayansi na kwamba kila mwaka wanafunzi 10 kutoka nchi 14 za Afrika watanufaika na udhamini huo.
Aidha Dk. Dinesh ameeleza kuwa
kampuni hiyo kama mdau wa mawasiliano wanachukua nafasi hiyo na kuingia
makubaliano ya kusomesha vijana hao kwa zaidi ya shilingi bilioni 1.3 kila
mwaka.
Kwa upande
wake Waziri Lela amesistiza haja ya taasisi na kampuni za mawasiliano kuwekeza
katika elimu ya vijana ili taifa lipate wasomi waliobobea katika fani mbali
mbali ikiwemo teknolojia.
Amesema programu hiyo ya pamoja kati ya IITMZ, Airtel Foundation na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inapaswa kupongezwa kwani itawawezesha vijana wa Afrika kupata elimu na ujuzi juu ya sayansi ya data na akili mnemba ambazo ni changamoto za dunia ya sasa.
“Serikali zetu zote mbili
zinachukua jitihada kuhakikisha inawawezesha vijana kuwa wataalamu wa fani
mbali mbali hivyo naomba makampuni mengine kuiga mfano wa Airtel kuwasadia
vijana wapate ujuzi na nchi kuwa na wataalamu watakaoendeleza nchi yao”, ameeleza
Waziri Lela.
Naye, Balozi Dey, amesema katika ulimwengu wa kidijitali, ufikiaji wa elimu bora katika nyanja za sayansi ya data na akili mnemba (AI) si anasa bali ni hitaji la kusukuma ukuaji wa uchumi, uvumbuzi na maendeleo.
Aidha, amesema mpango wa ‘Airtel
Africa Fellowship’ unalingana kwa karibu na maono ya India katika mustakabali
wa kidijitali.
“Tunapokaribia mwaka 2047,
maadhimisho ya miaka 100 ya uhuru wa India, tunajitahidi kuhakikisha kuwa
ujumuishaji wa kidijitali, ufikiaji wa teknolojia na elimu ya kiwango cha juu duniani
unafikia kila kona ya jamii yetu,” alisema.
Naye Naibu Waziri Kipanga, akizungumza kwa niaba ya Waziri Profesa Adolf Nkenda, aliipongeza Airtel tanzania kupitia Airtel Fondation kwa kuendelea kuiishika mkono serikali kwa kuwaelimisha vijana wa Tanzania na Afrika kwa ujumla.
“Jukumu la kuelimisha vijana ni la
serikali lakini peke yake haiwezi hivyo tunapopata wadau wa elimu kama Airtel
ina maana tunasogeza karibu na jamii fursa za kupata elimu na ujuzi
unaolinufaisha taifa”, alisema.
Sambamba na hayo alieleza kuwa
serikali itaendelea kutoa mikopo ya elimu ya juu, ufadhili kupitia mpango wa
‘Samia Scholarship’ na kuunga mkono juhudi za wadau wa elimu ili ndoto na
dhamira ya kupata wataalamu wazalendo ifikiwe.
Naye Katibu Mkuu wizara ya ujenzi na mawasilano, Mkame, alisema wizara hiyo inahudumia sekta ya mawasiliano ikiwemo kampuni ya Airtel ambao wameonesha mfano wa kuigwa kwa kampuni nyengine hivyo jamii inapaswa kutumia fursa hiyo kwa kujiunga na kozi za umahiri katika teknolojia, akili mnemba na ulinzi wa mitandaoni hatua itakayozalisha wataalamu wanaohitajika na nchi zao.
Comments
Post a Comment