PBZ yashukuru uwepo wa sera, sheria zinazokuza sekta za fedha
NA MWANDISHI WETU
BENKI ya watu wa Zanzibar (PBZ) imezishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa kuweka mazingira wezeshi yanayokuza biashara na kuimarisha sekta za fedha nchini.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi (wa tatu kulia) akipokea zawadi maalum kutoka kwa Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), Arafat Haji wakati wa hafla ya ufunguzi wa tawi jipya la benki hiyo wilayani Nyamagana mkoani Mwanza.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mwendeshaji wa benki hiyo, Arafat Haji Ali, wakati wa uzinduzi wa tawi la benki hiyo wilayani Nyamagana, mkoani Mwanza uliofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Arafat alieleza kuwa jitihada zinazofanywa na Rais Dk. Mwinyi na Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, za kubuni miongozo na sera zinazoimarisha ukuaji wa uchumi na kuchochea mafanikio ya taasisi za kifedha.
Alieleza kuwa PBZ ni benki ya saba kwa ukubwa kwa kuwa na rasilimali zaidi ya shilingi trilioni 2.3, inaendelea kutanua mtandao wake wa matawi ambapo kwa mwaka huu pekee imeweza kufikia mikoa mitatu mipya ya Morogoro, Mbeya na Mwanza.
Aliongeza kuwa katika kutekeleza mpango kazi wa benki hiyo wanatarajia kufungua matawi mengine katika mikoa ya Arusha, Tanga na mengine ya tanzania bara huku akibainisha kuwa mpaka sasa, huduma za benki hiyo zinapatikana maeneo yote kupitia kadi za VISA, Kadi za Umoja Switch, mawakala, simu za mkononi na mtandaoni kupitia ‘internet banking’.
Arafat alisema tawi hilo litawasaidia kwa kiasi kikubwa wananchi wa mkoa huo kupitia unafuu na ubora wa huduma za benki hiyo sambamba na fursa mbali mbali za uwezeshwaji na mikopo kwa makundi yote wakiwemo wakulima, wafugaji, wajasiriamali, wafanyabiashara, na wafanyakazi wote wa umma na binafsi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Dk. Mwinyi, alipongeza uamuzi wa benki hiyo kufungua matawi maeneo mbali mbali ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwani kufanya hivyo kunaongeza biashaba na kuwafikishia huduma wateja wake.
“Kuwepo kwenu hapa (Mwanza) sio tu kutaongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi wa mkoa huu na mengine ya jirani bali kutapanua wigo wa biashara za kibenki kupitia mikopo na huduma nyengine zinazotolewa na benki hii”, alieleza Dk. Mwinyi.
Aidha aliwahimiza wananchi wa Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa ujumla kuitumia vyema benki hiyo huku akiipongeza menejimenti na watendaji wa benki hiyo kwa kuendele na jitihada za kujitanua katika mikoa mbalimbali Tanzania bara ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kutekeleza kwa vitendo dhamira ya serikali ya kuwaunganisha wananchi wa pande zote mbili za muungano kiuchumi.
Hafla ya uzinduzi wa tawi hilo lililopo wilayani Nyamagana mkoni Mwanza, ulihudhuriwa na viongozi mbali mbali waandamizi kutoka Tanzania bara na Zanzibar akiwemo Mke wa Dk. Mwinyi, mama Mariam Mwinyi, Waziri wa Fedha wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mwigulu Lameck Nchemba na Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Dk. Saada Mkuya Salum.
Wengine ni Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais Ikulu, Zanzibar, Ally Suleiman Ameir, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi, Mwanaasha Khamis Juma, Mkuu wa wilaya ya Nyamagana, Amina Nassoro Makilagi huku Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya PBZ, Joseph Abdalla Meza aliwaongoza wafanyakazi wa benki hiyo katika hafla hiyo.
Comments
Post a Comment