Takukuru kuongoza vita dhidi ya rushwa SADC
NA MWANDISHI MAALUM, LUSAKA – ZAMBIA
TANZANIA kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), imechukua uongozi wa taasisi za mapambano dhidi ya rushwa katika ukanda wa Kusini mwa Afrika (SADC) ikiwa ni mara ya pili kushika nafasi hiyo.
Katika hotuba yake ya uzinduzi
wa mkutano wa mwaka wa Wakuu wa Mamlaka za
Kupambana na Rushwa kwa nchi za SADC, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin
Francis Chalalima (pichani), ambaye pia ni Mwenyekiti mpya wa kamati ya SADC ya kupambana
na rushwa (SACC), ametahadharisha kuhusu hatari ya rushwa kwenye utoaji wa
misaada wakati wa dharura.
Chalamila ameeleza kuwa majanga
ya dharura kama vile mlipuko wa magonjwa na athari za mabadiliko ya tabia nchi
yanaweza kufungua milango ya rushwa katika hatua mbalimbali za ugawaji misaada,
ikiwa ni pamoja na udanganyifu, ubadhirifu wa mali, na ukiukwaji wa maadili ya
ununuzi.
“Mchakato wa utoaji misaada upo
katika hatari kubwa ya kudhibitiwa na rushwa kwa sababu ya haraka na udharura
wa hali zinazokuwepo,” amesema Chalamila.
Aliongeza kuwa pia kunaweza
kutokea matumizi mabaya ya ngono (sextortion) kama mojawapo ya aina za rushwa
zinazoweza kutokea katika kipindi hicho.
Mkutano huo, ukiwa na kaulimbiu
isemayo ‘Kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa katika usimamizi wa majanga na
huduma za magereza katika ukanda wa SADC’, umeangazia changamoto zinazoikabili
nchi wanachama wa SADC katika kukabiliana na rushwa wakati wa kushughulikia
dharura.
Hivyo Chalamila alisisitiza
umuhimu wa kuwepo kwa mikakati imara ya kanda hiyo ili kuhakikisha misaada inawafikia
kwa walengwa kwa uadilifu na uwazi.
Aidha Chalamila alimpongeza
Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Monica Chipanta Mwansa wa Zambia, kwa uongozi
imara katika kutekeleza mpango mkakati wa SADC wa kupambana na rushwa wa mwaka 2023
- 2027, ambao umejikita katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuongeza
uwajibikaji katika usimamizi wa misaada na majanga.
Mkutano huo wa siku tatu,
uliofanyika jijini Lusaka, ulihudhuriwa na wawakilishi kutoka nchi 14 wanachama
wa SADC huku Tanzania ikiongoza mapambano hayo kwa mara ya pili baada ya kuwa Mwenyekiti
mwaka 2017/2018.
TAKUKURU inatarajiwa kuendelea na
juhudi hizi kwa mwaka wa 2024/2025, ikiwa mstari wa mbele katika kuhakikisha
ukanda wa SADC unakuwa na mazingira salama na huru dhidi ya vitendo vya rushwa.
Comments
Post a Comment