Dk. Samia ataka waumini kutumia nyumba za ibada kujijenga kiimani
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amewataka waumini wa madhehebu mbali mbali nchini kuhakikisha wanatumia nyumba za ibada kwa ajili ya kujijenga kiimani badala ya kugeuza kuwa maeneo ya kufanya vurugu na kusababisha uvunjifu wa amani.
Dk. Samia aliwataka wazazi hususani wanawake kuhakikisha wanatenga muda kwa ajili ya malezi ya watoto wao kwani kwa sasa watoto wengi wamekuwa wakiharibika kutokana na kutokuwa naa malezi mema.
Alisema hayo jana mjini Morogoro wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi wa msikiti wa Alghaith inayosimamiwa na taasisi ya The Islamic Foundation.
Alisema nyumba hizo za ibara ni vyema zikatumika kuunganisha kamba ya waumini na sio kukata kamba hiyo inayounganishwa na Mungu halafu wakajiita ni viongozi wa dini huku wakisababisha mifarakano kwa waumini wao na kuwataka kutofikia huko na kwamba binadamu huwa wanatofautiana.
Aidha alizungumzia suala la malezi ya watoto aliwataka wazazi hususani akima mama kuhakikisha wanatenga muda wa kutosha kwa ajili ya malezi ya watoto badala ya kutegemea wababa ambao ndio wamekuwa wakiogopwa na watoto kwa sasa.
Alisisitiza akina mama hao kukaza kamba katika suala zima la malezi yanayofaa ambayo yanakwenda sambamba na imani kwa kusimamia misingi ya malezi bora.
Alisema pamoja na ujenzi wa Misiki kuendelea ni vyema yakajengwa pia Madrasa za kutosha zitakazosaidia kutoa elimu kwa watoto ili kuwa na jamii yenye maadili mema na kumjua Mungu.
Akatoa rai kwa raasisi hiyo kuendelea kutoa michango yake kwenye jamii husussani kwenye sekta za afya, elimu na maji na ni sadaka nzurim ambapo alisema maji ni uhai na binadamu anahitaji afya njema hivyo vitu hivyo ni muhimu kwa jamii.
Kwa upande wake, waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, alisema pamoja na serikali kusimamia vyombo vya ulinzi na usalama katika suala zima la kulinda amani na utulivu lakini pia taasisi za dini zina mchango mkubwa katika kulinda amani na utulivu wa nchni hiyo.
Masauni alisema baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakitumia kipindi hiki cha uchaguzi kushawishi wananchi kujiingiza katika vurugu na kupelekea uvunjifu wa amani ambapo aliwataka kujiepusha na hali hiyo ili kuendelea kufaidi matunda ya nchi.
Rais wa Taasisi ya The Islamic Foundation, Arif Nahad awali akizungumza wakati wa uwekaji huo wa jiwe la msingi alisema mradi huo ulianza ujenzi wake mwaka 2021 na mpaka sasa umefikia asilimia 80 ambapo mkapa kukamilika kwake itaghalimu kiasi cha shilingi bilioni 7.
Nahad alisema kukamilika kwa mradi huu wa msikiti utaweza kuhudumia waumini wapatao elfu tatu kwa wakati mmoja na kwamba msikiti huo utakuwa na huduma mbalimbali ikiwemo ya kuhifadhia na kuosha maiti, maktaba ya kisasa, nyumba za kupumzikia mashehe na madrasa.
Aidha Nahad alisema mpaka sasa Taasisi imefanikiwa kujenga Misikiti zaidi ya 1,600 maeneo mbalimbali nchini kwa bara na Visiwani, ambapo misikiti hiyo ina madrasa zenye wanafunzi takribani elfu themanini (80,000).
Pia alisema taasisi hutoa huduma ya maji safi na salama kwa jamii kwa kuchimba visima virefu na vifupi ambapo kwa sasa taasisi imefanikiwa kuchimba visima zaidi ya 3,000 kwenye maeneo mbalimbali Tanzania bara na Visiwani.
Akizungumzia sula la malezi Nahad alisema wazazi wa sasa wanatakiwa kubadilika kwa kufuata maadili, na kwamba nyumba za ibada itasaidia kwa kiasi kikubwa watoto kubadilika kwa kuwafundisha maadili mema.
Comments
Post a Comment