Nsokolo ajiuzulu urais UTPC
NA MWANDISHI WETU
RAIS wa Muungano wa klabu za waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Deogratius Nsokolo (pichani) amejiuzulu wadhifa huo kufuatia kupata uteuzi wa kutumikia taasisi nyengine ya kisiasa hivi karibuni.
Nsokolo aliyekuwa akikamilisha kipindi cha pili cha uongozi wake katika nafasi hiyo, alifikia uamuzi huo Novemba 10, mwaka huu na kwamba Makamu wake, Pendo Mwakyembe atakaimu nafasi ya Rais hadi utakapofanyika uchaguzi mkuu wa taasisi hiyo inayoundwa na klabu 28 za waandishi wa habari nchini.
Taarifa iliyotolewa kwa viongozi wa klabu za wanahabari Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC, Keneth Simbaya hivi karibuni na, ilithibitisha kupokea barua ya kujiuzulu kwa kiongozi huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa Habari Kigoma na mwandishi wa kituo cha televisheni ya ITV mkoani humo.
Kaimu Rais wa UTPC, Pendo Mwakyembe
“Napenda kuwafahamisha kuwa tumepokea rasmi barua ya kujiuzulu kwa Rais wa UTPC, Deogratius Nsokolo tarehe 10 Novemba, 2024 baada ya kupata uteuzi na wadhifa ambao kuendelea na kazi yake ya Urais kungekinzana na katiba ya UTPC”, ilieleza taarifa ya Simbaya.
Aidha aliwaomba viongozi wa klabu kuelekeza mambo yote kwa Kaimu Rais wa UTPC, Pendo Mwakyembe, huku akimshukuru na kumpongeza Nsokolo kwa uteuzi na uamuzi wake wa kuheshimu katiba ya UTPC jambo linaloonesha ukomavu katika uongozi.
Vile vile Simbaya aliwaomba viongozi, wanachama na wanahabari nchini kumtakia kheri kiongozi huyo aliyekuwa akikamilisha kipindi cha pili cha urais wa UTPC katika majukumu na wadhifa wake mpya.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Nsokolo aliwashukuru wanachama na viongozi wa klabu za waandishi wa habari kwa ushirikiano waliompa katika kuiongoza taasisi hiyo na kuahidi kuendelea kutambua mchango wao uliochangia kupata uteuzi huo.
Nsokolo
ambaye Novemba 1 na 2, mwaka huu aliongoza mkutano mkuu wa UTPC ulioambatana na
maadhimisho ya siku ya kumaliza madhila (uhalifu) kwa waandishi wa habari duniani na
tunzo za uadilifu kwa waandishi wa habari wanawake na wanaume matukio
yaliyofanyika mkoani Singida, ameteuliwa kuwa Katibu wa Idara ya Siasa na Uenezi
ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoa wa Kigoma.
Comments
Post a Comment