Programu ya IMASA kuwanufaisha wananchi, wajasiriamali wadogo – Ayoub
NA MWANDISHI MAALUM
MKUU wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud, akifungua programu ya Imarisha Uchumi na Mama Samia (IMASA) mkoani humo katika ukumbi wa Dk. Ali Mohamed Shein Tunguu. Programu hiyo inasimamiwa na Baraza la Uwezeshaji Tanzania (NEEC) kwa kushirikiana na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA).
Alisema kwa muda mrefu wananchi wamekuwa wakipata uwezeshaji kwa miundombinu mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara, afya, Maji na miundombinu nyengine lakini dhamira ya Dk. Samia na Dk. Hussein Ali Mwinyi ni kuwanufaisha wananchi wenye kipato cha chini kiuchumi na kuondokana na umasikini.
Aidha alisema wananchi wa mkoa wa Kusini wanafarajika kupewa heshima hiyo kwani programu hiyo ni dhamira njema ya Rais Samia ambae anatoka katika mkoa huo kuwawezesha kiuchumi kwa kuweza kujiajiri na kuajiri wengine.
Ayoub alibainisha kuwa mchakato wa uwezeshaji kupitia IMASA ni muhimu hivyo aliwasisitiza wanakusini wasichezee fursa hiyo bali ni kuitunza na kuidumusha kwa kumuunga mkono Dk. Samia kwa hali na mali ili waendeleee kupata fursa hizo na nyengine kwa ujumla.
BAADHI ya watendaji kutoka ZEEA na taasisi za serikali, wakifuatilia ufunguzi wa programu ya Imarisha Uchumi na Mama Samia (IMASA) kwa mkoa wa Kusini Unguja.
Alisema kwa mkoa huo programu hiyo itahusisha watu 700 watakaopunguza changamoto ya maisha kwa watu zaidi ya 30,000 kwa Zanzibar kwani hiyo ni dhamira njema ya Rais kwa wananchi wake.
Hivyo, aliyaomba makundi yaliyochaguliwa katika program hiyo wakiwemo wanawake, wazee, vijana na watu wenye ulemavu kutumia fursa hiyo kwani ndio makundi yanayoongoza katika umasikini.
Naye Katibu Mtendaji Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng'i Issa, akitanbulisha programu hiyo alisema Dk. Samia anakusudia kuwakomboa kiuchumi wananchi kupitia programu hiyo iliyolenga kuwatoa walipo wajasirimali na kupata mafanikio zaidi.
Alisema programu hiyo imelenga kunufaisha makundi ya wanawake, vijana wazee na watu wenye ulemavu hivyo mtu shughuli yake anayoifanya ni lazima kufanya kwa weledi.
Hata hivyo alisema pia watasajiliwa kupitia simu zao za mkononi kwa kutumia simu janja na wale ambao hawana simu Basi pia watajisajili kuingia katika program hiyo ya IMASA.
Akizungumza mpango wa kuwawezesha wananchi, Mkurugenzi wa Wakala wa UwezeshajiWananchi Kiuchumi (ZEEA), Juma Burhan, alisema ZEEA inajukumu la kuwawezesha wananchi katika idara ya mikopo na uwezeshaji, mafunzo na masoko na idara ya viwanda.
Alisema mkoa huo bado upo nyuma katika kuomba mikopo kwani wameshatoa shilingi bilioni 33 lakini mkoa huo umepokea bilioni 1.2 na wakala huo una mikopo ya aina tatu ukiwemo wa programu ya Inuka unaotoa shilingi milioni 2 hadi milioni 50 kupitia benki ya CRDB.
“Pia kuna programu ya makundi maalum FF2 kupitia fedha za halmashauri asilimia 10 na program milioni 2 hadi 30 kupitia benki ya TCB ambao tayari wameshapatiwa bilioni 1.8 na programu ya wajasiriamali wadogo, wadogo wadogo na wakati kutoka milioni 2 hadi milioni 200 kupitia Abudhabi Fabdi”, alieleza mkurugenzi huyo.
Hata hivyo alisema mwaka uliopita ZEA ilipatiwa shilingi bilioni 15 na tayari zimeshafikia bilioni 33 ambapo katika bajeti ya mwaka huu imepewa shilingi bilioni 41.6 hivyo hakuna sababu ya wajasirimali kukosa mikopo hiyo ambayo haina riba.
Alisema hizo ni fursa zinazotolewa na SMT na SMZ kupitia viongozi wakuu wa nchi kwa nia zao safi za kuwasaidia wananchi kukua kimaendeleo ambapo mikopo hiyo ipo kwa ajili yao na hakuna sababu ya kuikosa hivyo ni vyema kuzikimbilia fedha hizo ili waweze kuinuka kiuchumi kwa kufuata sheria na muongozo ya kupata mikopo hiyo.
Hivyo aliwaomba kuwashajihisha wengine kuingia katika mfumo huo na wakala utahakikisha unaendelea kuwasajili watu ili kuweza kuwaambua na biashara zao wanazozifanya kwani unasiriamali inaweza kumuinua mtu kiuchumi.
Comments
Post a Comment