Upigaji kura ‘Samia Kalamu Awards’ waanza rasmi
NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
ZOEZI la upigaji kura kwa washiriki wa tuzo Samia Kalamu Awards, limeanza Novemba 11 na litakamilika Novemba 20, mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari, upigaji kura utahusisha wananchi kwa asilimia 60 ya matokeo kwa kuwa ndio walaji wa maudhui na asilimia 40 ya alama za vigezo vya kitaaluma zitatolewa na jopo la majaji.
Watakaopigiwa kura ni wanahabari na vyombo vilivyokidhi vigezo vya kitaaluma vya uandishi wa habari za maendeleo ambapo makala 1,131 ziliwasilishwa kutoka mikoa yote ya Tanzania bara na Zanzibar kuwania tuzo hizo.
Aidha chambuzi za kitaaluma 85 zilizokidhi vigezo ambazo zimewekwa tovuti ya Samia Awards na mitandao ya kijamii pia zitapigiwa kura.
Taarifa hiyo imesema tuzo hizo zinalenga kuhamasisha, kukuza na kupanua wigo wa uandisi, utangazaji na uchapishaji wa maudhui ya ndani kupitia vyombo vya habari vya asili na mtandaoni ili kuchochea uandishi wa makala za kina zinazozingatia maendeleo, uwajibikaji, mila na tamaduni.
“Tunawahimiza wananchi na wadau wa habari kushiriki katika mchakato huu wa kupiga kura na tuzo zimegawanywa katika makundi makuu matatu ambayo ni tuzo maalum za kitaifa, tuzo za vyombo vya habari na tuzo za kisekta,” ilisema taarifa hiyo.
Comments
Post a Comment