SMZ yabariki uwekezaji wa Puma Energy sekta nishati
NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Shaib Hassan
Kaduara ameipongeza Puma Energy Tanzania kusogeza huduma ya nishati ya mafuta
na huduma za ziada kwa wananchi wa Zanzibar baada ya kuzindua kituo cha kuuza
mafuta Unguja visiwani Zanzibar.
Aliishukuru bodi ya wakurugenzi wa kampuni hiyo kwa uamuzi wa kupanua uwekezaji wao Zanzibar ambao umelenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya nishati ya mafuta ya gari karibu na maeneo yao sambamba na kuunga mkono jitihada za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kufungua uchumi na kuleta maendeleo.
Aidha Waziri Kaduara aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kuwa mshirika wa kampuni hiyo wakati wote na kuongeza siku zote wamekuwa tayari kutathimini fursa na mipango mipya ya kuwahudumia wananchi katika sekta ya nishati.
Kaduara amesisitiza kuwa hatua ya Puma Energy Tanzania kuzindua kituo hicho cha mafuta inaashiria hatua nyingine ya maendeleo ya sekta ya nishati Zanzibar na ni uthibitisho wa ushirikiano wenye kuleta tija kati ya Serikali na wadau wa sekta binafsi kama Puma Energy Tanzania .
Akieleza zaidi amesema kituo cha mafuta cha Puma Energy Tanzania katika visiwa hivyo kitatumika kama kielelezo cha uwekezaji kwa siku zijazo zikionesha uwezo na ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi katika kuchochea ukuaji wa maendeleo ya shughuli za kijamii na kiuchumi hapa Zanzibar
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Fatma Abdallah, amesema kampuni hiyo imekuwa ikitoa huduma Zanzibar tangu mwaka 1994 na wakati wote huo wamekuwa wakitoa huduma ya kuuza mafuta ya ndege na sasa wamezindua kituo cha mafuta kwa ajili ya vyombo vya moto yakiwemo magari.
“Tunatoa shukrani kwa Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na kuongeza uchumi wa Zanzibar kwa kuhakikisha unaendelea kukua kwa kasi.Kutokana na mazingira mazuri ya uwekezaji dhamira yetu ikiwa ni kuendelea kuongeza vituo mafuta Unguja na kwa Pemba tunatarajia ifikapo mwaka 2025 tuwe na kituo cha mafuta”, amesema Mkurugenzi huyo.
Aidha Fatma amesema kimetumia zaidi ya shilingi bilioni 2.5 hadi kukamilika kwake na kimetoa ajira kwa wananchi wanaozunguka.maeneo ya Fuoni na kusisitiza kituo hicho kitatoa huduma katika Viwango vya Kimataifa.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya kampuni hiyo, DkSelemani Majige, amesema kampuni hiyo inajivunia ubora wa bidhaa zake na kuongeza mkakati wao kwa Zanzibar ni kuendelea kusogeza huduma zake visiwani Zanzibar.
Pia amewaomba wananchi wa Zanzibar kuendelea kuungana katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo kwa pande zote mbili za muungano za Tanzania Bara na Zanzibar.
“Tunawaomba wananchi wa Zanzibar kuja katika kituo hiki kununua mafuta ambayo ni bora na mkakati wetu Puma Energy Tanzania ni kuendelea kusogeza huduma na bidhaa zetu kwa wananchi”, amesema.
Comments
Post a Comment