SMZ yawaita vijana kushiriki kilimo
NA MWANDISHI WETU
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imewahimiza vijana nchini kubadili mitazamo yao juu ya kilimo kwani ni miongoni mwa kazi zenye faida na tija kiuchumi na kijamii.
Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Shamata Shaame Khamis, alitoa wito huo hivi karibuni baada ya kuzindua awamu ya pili ya mradi wa uendelezaji kilimo unaofadhiliwa na Serikali ya watu wa Marekani na serikali ya Jamhuri ya watu wa Korea Kusini, huko Kibokwa mkoa wa Kaskazini Unguja.
Shamata alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinashirikiana na washirika wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi ili kutekeleza mikakati inayohakikisha vijana na wanawake wanawezeshwa na kutumia fursa zilizomo kwenye kilimo.
Aliongeza kuwa kupitia programu na mikakati mbali mbali, vijana wamewezeshwa kumiliki biashara za kilimo na miundombinu ya uzalishaji kuzalisha mazao yanayohitajika kwenye hoteli za kitalii na masoko mengine ya ndani.
“Hatua hii si tu inalenga kupunguza wimbi la ukosefu wa ajira kwa vijana wetu bali pia kuongeza nguvu kazi kwenye uzalishaji wa chakula ili kupunguza uagizaji wa bidhaa za chakula toka nje ya nchi”, alieleza Shamata.
Aidha alipongeza ufadhili unaotolewa na Serikali ya Watu wa Marekani na ya Jamhuri ya Watu wa Korea Kusini ambao umeimarisha uzalishaji wa mazao na kuboresha maisha ya wakulima wa Zanzibar kupitia teknolojia na mafunzo ya kisasa.
"Tunaamini kuwa ushirikiano huu utasaidia Zanzibar kufikia malengo yake ya maendeleo endelevu katika sekta ya kilimo na kuwawezesha wakulima kuongeza uzalishaji kwa njia rafiki kwa mazingira", alisema Shamata.
Kwa upande wake Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Michael Battle, alipongeza juhudi zinazochukuliwa na serikali za Tanzania katika kuimarisha uzalishaji na upatikanaji wa chakula jambo linaloihakikishia nchi usalama na kuimarika kiuchumi.
Alieleza kuwa kupitia mradi wa Feed the Future; Imarisha sekta binafsi na Kilimo tija, inayotekelezwa na Shirika la Misaada ya Maendeleo Kimataifa (USAID), Marekani itaendelea kutoa usaidizi kwa makundi ya vijana na wanawake ili kujiimarisha kwa kulima kisasa na kuongeza thamani ya kilimo.
Alieleza kuwa miradi hiyo inakuza ushirikiano wa kibunifu kati ya sekta ya umma na sekta binafsi na kuimarisha uhusiano na sekta binafsi jambo linalopelekea wanawake na vijana tayari kuzalisha mwaka mzima.
“Chini ya mipango ya kilimo cha mkataba na hoteli za ndani za Zanzibar, wanawake na vijana hawa wanaongeza mapato yao kwa kiasi kikubwa huku wakionesha nguvu ya umwagiliaji bora ili kubadilisha kilimo Zanzibar”, alieleza Balozi Battle.
Naye Balozi wa Korea Kusini nchini Tanzania, Eunju Ahn, alisema kuwa mradi wa kilimo cha umwagiliaji visiwani Zanzibar, ulioanzishwa mwaka 2019 umeongeza eneo la kilimo na kuwa nguzo muhimu katika kuinua sekta ya kilimo.
Alieleza kuwa mradi huo ni sehemu ya jitihada za Korea Kusini kusaidia maendeleo ya kilimo zajnzibar unaohusisha mabonde ya Kinyasini, Cheju, Kibokwa, Kilombero, na Chaani.
"Tangu mwaka 2019, mradi huu umeboresha kilimo cha umwagiliaji kupitia ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji yenye jumla ya kilomita 104 kwa kila eneo na kufadhili takribani dola milionI 4 za kimarekani," alisema Balozi Eunju.
Aidha Balozi Ahn alisisitiza dhamira ya nchi kuendelea kushirikiana na serikali ya Zanzibar na marekani kupitia mradi wa Feed the Future Tazanzia kuimarisha sekta binafsi na kuhakikisha kilimo kinakuwa msingi wa maendeleo endelevu ya nchi na watu wake.
Comments
Post a Comment