Watendaji, wadau wa uchaguzi wapatiwa mafunzo ya uboreshaji daftari

WATENDAJI wa uchaguzi na wdau wa uchaguzi wa mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Dodoma wamepatiwa mafunzo kujianda na zoezi la  uboreshaji wa daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

hatua hiyo ni maandalizi ya zoezi la uboreshaji wa daftari hilo katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Halmashauri za Wilaya ya Kondoa, Kondoa Mji na Chemba linalotarajiwa kuafanyik Disemba 11 - 17, 2024.

Akifungua mafunzo hayo jijini Arusha, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji wa Mahakama ya Rufaa Jacobs Mwambegele (pichani juu), amesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa watendaji hao kwa sababu ujuzi na elimu watakayopata itawawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kufanikisha uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.

“Mafunzo haya yanalenga kuwajengea umahiri watendaji wetu ili waweze kuwafundisha Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Kata, ambao nao watatoa mafunzo kwa Waendeshaji wa Vifaa vya Bayometriki na Waandishi Wasaidizi, ambao ndio watakaohusika moja kwa moja na uandikishaji wa wapiga kura katika vituo”, amesema Jaji Mwambegele.

VIONGOZI wa vyama vya siasa, Dini, Wawakilishi wa Asasi za Kiraia, Wahariri wa Vyombo vya habari, Waandishi wa habari, Maafisa Habari wa mikoa na Halmashauri, Wawakilishi wa makundi ya vijana, watu wenye ulemavu, wanawake na wazee wa Kimila wakiwa kwenye mkutano wa wadau wa uchaguzi. 

Jaji Mwambegele amesisitiza umuhimu wa kutumia uzoefu wa watendaji waliowahi kushiriki katika mchakato wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, ili kusaidia wenzao ambao hawajawahi kushiriki katika zoezi kama hili, na kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Katika mkoa wa Kilimanjaro, mafunzo kwa watendaji wa uchaguzi ngazi ya mkoa yalifunguliwa na Makamu Mwenyekiti wa INEC, Jaji Mstaafu Mbarouk Salim Mbarouk ambaye amesisitiza kuwa mawakala wa vyama vya siasa wataruhusiwa kuwepo katika vituo vya kuandikishaji wapiga kura, lakini ameonya kuwa hawataruhusiwa kuingilia mchakato wa uboreshaji wa daftari la kudumu.

MAKAMU Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu wa mahakama ya Rufaa, Mbarouk Salim Mbarouk, akifungua mafunzo ya Waratibu wa Uandikishaji wa mkoa, Maafisa Waandikishaji, Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ugavi na Maafisa TEHAMA wa halmashauri mkoani Kilimanjaro

“Kwa madhumuni ya kuleta uwazi, mawakala wa vyama vya siasa watasaidia kutambua waombaji wapiga kura katika maeneo yao, jambo litakalosaidia kupunguza vurugu zisizohitajika” amesema Jaji Mbarouk.

Aidha ameongeza kuwa ni muhimu kwa watendaji wa uchaguzi kutoa ushirikiano kwa mawakala hao na kuhakikisha maelekezo ya Tume yanafuatwa ipasavyo.

Katika mafunzo yalifanyika mkoani Dodoma, Mjumbe wa Tume hiyo, Jaji wa Mahakama Kuu, Asina Omari, alifungua mafunzo hayo katika ukumbi wa Mkuu wa mkoa wa Dodoma na kusisitiza umuhimu wa utunzaji wa vifaa vya uandikishaji, akisema kuwa kutokuwa makini katika utunzaji wa vifaa hivyo kutapelekea athari kubwa katika ukamilishaji wa zoezi hili muhimu.

“Vifaa vya uandikishaji vimenunuliwa kwa gharama kubwa, hivyo ni lazima tuvisimamie kwa umakini na kuhakikisha vinatumika ipasavyo katika maeneo yote ya uandikishaji”, amesema Jaji Asina.

Mafunzo hayo yamehudhuriwa na maafisa waandikishaji, maafisa TEHAMA na maafisa ugavi kutoka halmashauri za mikoa hiyo ambao walipatiwa ujuzi wa jinsi ya kutumia mfumo wa ‘Voters Registration System’ (VRS) pamoja na vifaa vya kisasa vitakavyotumika katika vituo vya kuandikishia wapiga kura pamoja na kufundishwa namna ya kukabiliana na changamoto za kiufundi zinazoweza kutokea wakati wa zoezi la uandikishaji. 

Comments

Popular posts from this blog

Balozi Mpanda ahimiza ubunifu uhifadhi wa mazingira

ZAMECO yakerwa na video ya udhalilishaji mtandaoni