Watoa huduma 100, wanafunzi 500 wa Muhimbili wapatiwa chanjo homa ya ini

#KaziInaongea

SERIKALI ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan, kupitia Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, hivi karibuni imefanya vipimo na kutoa chanjo ya Homa ya Ini kwa watoa huduma za afya 100 wa Kitengo cha dharura Hospitali ya Taifa Muhimbili na
wanafunzi 500 wa Chuo cha Sayansi Muhimbili (MUHAS).

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Mohamed Janabi, amesema kuwa, Muhimbili kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), wamezindua mpango wa kuwapatia chanjo dhidi ya Virusi vinavyosababisha Homa ya Ini (Hepatitis B Vaccine) kwa wafanyakazi hao na wanafunzi Chuo Kikuu cha Afya cha Muhimbili (MUHAS).

“Leo nimeshiriki uzinduzi wa zoezi la upimaji na chanjo ya homa ya Ini kwa watoa huduma za afya kitengo cha dharura Hospitali ya Taifa Muhimbili na wanafunzi wa Chuo cha Sayansi Muhimbili”, amesema Prof. Janabi.

Amefafanua kuwa, chanjo hii ni muhimu sana kwa watoa huduma za afya ambao wako kwenye hatari mara 10 zaidi ya kupata maambukizi ya Homa ya Ini ikilinganishwa na watu wa kawaida.

Kwa mujibu wa WHO, mwaka 2022, zaidi ya watu Milioni 254 walikuwa wakiishi na maambukizi sugu ya Homa ya Ini, na zaidi ya watu Milioni moja walifariki kutokana na magonjwa yanayohusiana nayo kama saratani ya ini.

Aidha Dk. Janabi amewasihi wananchi kuchukua hatua sasa ya kujikinga na ugonjwa huo kwa kupata chanjo, ambayo ni salama, bora na rahisi kupatikana.

 

Comments

Popular posts from this blog

ZAMECO yakerwa na video ya udhalilishaji mtandaoni

Airtel Foundation yazindua mpango wa udhamini wa masomo kwa vijana

SMZ yawaita vijana kushiriki kilimo